RAIS JK KUSHUHUDIA MTANANGE WA WABUNGE v WAKUU WA WILAYA ITAKAYOPIGWA UWANJA WA TAIFA JUNI 29

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mechi ya hisani itakayowakutanisha waheshimiwa wabunge na Wakuu wa wilaya, itakayopigwa Juni 29, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya Juni 22 mjini Dodoma, ambapo huko mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambapo lengo la mechi hizo ni kuchangisha fedha za ujenzi wa shule ya albino, huku kukipangwa kuwa na burudani za kila aina, sambamba na wasanii watakaoamua kuungana na serikali juu ya uchangiaji huo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa timu hiyo ya wakuu wa wilaya, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema kuwa huku mheshimiwa rais akiwa mgeni rasmi, ila wamejipanga imara kwa ajili ya kuwaonyesha kazi wabunge, ambao baadhi yao wameanza kujigamba dhidi ya mechi hiyo ya aina yake.
Alisema kuwa Watanzania wote watakaopata fursa ya kuhudhuria kwenye mechi hizo wataaburudika kwa kiasi kikubwa, huku wakiamini kuwa licha ya wakuu wa wilaya wengi kuwa mikoani, ila wana nguvu na ari ya kushinda mbele ya wabunge.
“Tupo imara na tutaanza mazoezi yetu kesho Jumatatu kwa kukutanisha wakuu wa wilaya wote waliokuwa kwenye timu hii, huku barua za kuwaombea mialiko kutoka kwa Wakuu wa Mikoa tayari zimeshafika kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili.
“Katika mechi hizi, mwamuzi wa kati atakuwa atakuwa Reginald Mengi, ambaye ni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, huku waamuzi wa pembeni wakiwa ni IGP Said Mwema na Stephen Wassira, ambapo wote watashiriki katika mchezo huu,” alisema.
Aliwataja Wakuu wa wilaya waliotwa kwenye uundwaji wa kikosi hicho kuwa ni pamoja na Venas Mwamoto (Kibondo), Ramadhan Maneno (Kigoma), Norman Sigara (Mbeya), Krispin Meela (Rungwe), Benson Mpesya (Kahama), Deodatus Kinanilo (Chunya), Herman Kapufyi (Same), Francis Isaac ( Chemba), Wilson Mkambaku (Kishapu), Yahya Nawanda (Iramba), Elibariki Kingu (Igunga), Festo Kiswaga (Nanyumbu), Paza Mwamlima (Mpanda), Abdallah Ulega (Kilwa), Seleman Mzee (Kwimba), John Mongela (Arusha), Konstantin Kanyasu (Ngara), Paulo Mzindakaya (Busega), Mrisho Gambo (Korogwe), uhingo rweyemamu handeni, Cristofa Magala( Newala), Erasto Sima (Bariadi), Jordan Rugimbana (Kinondoni), Joseph Mkirikiti (Songea), Ngemela Rubinga (Mpanda) nay eye mwenyewe anayotokea wwilaya ya Handeni, ambaye pia ni msemaji wa timu hiyo.
Aidha, Muhingo alitaja kikosi cha wanawake kuwa kinaongozwa na Beth Mkwasa (Bahi), Sarah Dumba (Njombe), Josephine Mapiro (Makete), Hafsa Mtasiwa (Pangani), Mboni Mgaza (Mkinga), Halima Dendegu (Tanga), Queen Mlozi (Singida), Angelina Mabula (Butiama), Merry Tesha (Ukerewe), Christina Mndeme (Hanang), Anna Magoha (Urambo) Jacqueline Liana ( Magu).

Comments