MISS KIGAMBONI KUONDOKA NA 500,000, SHINDANO NI KESHO NAVY BEACH

Na Mwandishi Wetu
MREMBO atakayefanikiwa kutwaa taji la kitongoji cha  Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika kesho usiku kwenye ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni atajinyakuliwa kitita cha Sh. 500,000 imeelezwa.
Maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na warembo 12 kutoka sehemu mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Akizungumza na gazeti hili Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa mrembo atakayeshika nafasi ya pili katika shindano hilo atapata zawadi ya Sh. 300,000, mshindi wa tatu Sh. 250,000 huku wawili watakaotangazwa kushika nafasi ya nne na ya tano kila mmoja ataondoka na Sh. 200,000.
Somoe alisema kuwa warembo wengine saba waliobakia kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh. 100,000.
“Najua wote ni warembo na wanasifa ya kutwaa taji hilo lakini ni msichana mmoja tu ndiye atakayetangazwa mshindi wa shindano hilo, tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kuja kushuhudia safari ya Redd’s Miss Tanzania ikianzia Kigamboni leo,” Somoe alisema.
Aliitaja bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza katika shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh. 10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000.
Aliwataja warembo hao watakaochuana kuwa ni pamoja na Rogathe Michael, Irene Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa, Ellen Sulle, Joyce Kamtonosye na Zuhura Masoud.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Taji la Redd’s Miss Kigamboni linashikiliwa na Edda Sylivester ambaye pia ndiye mshindi wa kanda ya Temeka na alishika nafasi ya tatu katika shindano la Redd’s Miss Tanzania mwaka jana.
Wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd's Premium Original, Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z , Silver Boutique, Jambo Leo, Machapta Production na Logikit.