Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na
Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu)
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi
zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa
wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.
Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia
kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge
Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika
michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake
tutaukumbuka daima.
Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa
upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya
Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.
Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi
kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye
alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.
Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu
na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa,
Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es
Salaam.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na
kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments
Post a Comment