MAKOCHA WA STARS, IVORY COAST KUTETA NA WANAHABARI KESHO

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inayodhamini Timu ya Taifa (Taifa Stars) akisalimiana na mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu wakati wa hafla fupi ya kuzungumza na wachezaji jana kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki.

Wakati timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao. 
Mkutano huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast imefanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya Gymkhana. 
Timu zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9 kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9 kamili alasiri. 
Wakati huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana (Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na Uwanja wa Taifa. 
Mauzo yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa sh. 50,000 katika ofisi za TFF.