LIEWIG AKOMAA NA SIMBA SC, RAGE KUKUTANA NAYE JUMAPILI

WAKATI aliyekuwa kocha wa Simba  Mfaransa Patrick Liewig akitua nchini jana na kudai hatambui kutimuliwa kwake kazi, uongozi wa Simba umesema kocha huyo ni muongo kwani tayari alishakabidhiwa barua. 
Simba ilimtimua kukatisha mkataba wa mwaka mmoja wa kazi wa kocha huyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wake baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa ligi kuu bara na timu kuishia nafasi ya tatu. 
Akizungumza jijini jana, Liewing alisema anatambua bado ana mkataba na wekundu hao wa Msimbazi unamalizika hadi mwezi juni  hivyo amerejea kuendelea na kibarua chake baada ya mapumziko mafupi. 
Alisema wakati anaondoka uongozi haukumpa taarifa kama unaachana naye na ndiyo maana aliacha vitu vyake katika hoteli aliyokuwa akiishi na kama wangemwambia ukweli angecxhukua kila kilicho chake. 
Hata hivyo, Liewig alikiri kufahamu kuwa nafasi yake kwa sasa imechukuliwa na kocha mwingine na kuongeza kuwa baada ya kulifahamu hilo alizungumza na mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage  ambaye alimuahidi kuonana naye ili kutatua tatizo lake. 
“Kama kweli wameamua kuachana na mimi ni bora wanilipe changu ili tuachane vizuri kwani sitaki matatizo na mtu, hivyo nasubiri kuonana na mwenyeki (Rage) kama tulivyokubaliana na baada ya hapo nitajua nini hatima yangu,”alisema Liewig 
Sports Lady Blog ilipomtafuta Rage, alikiri kufahamu ujio wa kocha huyo sambamba na kupanga kukutana naye mwishoni mwa wiki. 
Hata hivyo, Rage alishangazwa na madai ya kocha huyo kutokuwa na taarifa za kutimuliwa kwake kwa madai kwamba analifahamu hilo na walimpatia barua kabla ya kwenda kwao. 
“Nilizungumza naye kabla hajaja na nimepanga kukutana naye jumapili, hivyo nitakutana naye na kumsikiliza shida yake ni nini juu ya Simba na baada ya hapo tutaangalia kama tutaitatua au la,”ALISEMA Rage

Aklienda mbali zaidi, Rage alisema kama ni suala la malipo ya kuvunja mkataba ni jambo la kawaida na haoni ajabu kwa Simba kudaiwa fedha na mtu ama taasisi yoyote, hivyo ni jambo la kuwa na subira.

“Sisi mbona tunaidai Etoile Du Sahel dola 300,000 za Emmanuel Okwi lakini kwa vile wametutaka tusubiri basi hatuana budi kusubiri,”aliongeza Rage


Baada ya kumtema Liewig ambaye alirithi mikoba ya Mserbia Milovan Cirkovic, Simba iliamua kumpa jukumu la kukinoa kikosi kocha mzawa Abdallah ‘King’ Kibaden ambaye anasaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’

Comments