KUELEKEA MECHI YA STARS V IVORY COAST:KILIMANJARO LAGER YATAKA WATANZANIA WASIKATE TAMAA

Na Mwandishi wetu
Wadhamini wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager wamewaomba watanzania washikane na kuungana pamoja wakati wa mechi dhidi ya Ivory Coast kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwani kuna watanzania ambao tayari wamekata tamaa.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe (pichani)alisema Taifa Stars inatakiwa kuungwa mkono na kushangiliwa kwa nguvu kwani wachezaji wameonesha kuwa wana uwezo.
“Hawa ni wanajeshi wetu…nawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi…tuwape sapoti na tuoneshe uzalendo kwani kwenye mpira lolote linawezekana,” alisema.
Bw Kavishe alisema watanzania lazima welewa timu hii bado ni changa na ina wachezaji wapya wenye umri mdogo ambao wameonesha uwezo mkubwa.
“Hata ikitokea tusifuzu kwenda Kombe la Dunia, vijana wameshaonesha dalili nzuri na tuna imani tutafanya vizuri katika mashindano mengine kama AFCON na CHAN,” alisema.
Aliwataka wachezaji kutulia uwanjani na kutobabaishwa na ukubwa wa timu ya Ivory Coast kwani wana uwezo wa kuwafunga na kushangaza dunia nzima Jumapili.
“Hii ni kama fainali kwa Ivory Coast na wao pia wamebabaika na kuitilia maanani kabisa mechi hii kwa sababu tukiwafunga ina maana hawatakuwa na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata,” alisema Kavishe.
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetimiza mwaka mmoja tangu ianze kuidhamini Taifa Stars na wadau mbalimbali wamesifia udhamini huu kwani umeleta mabadiliko makubwa katika timu ya Taifa.
Timu ya Ivory Coast iliwasili nchini Alhamisi usiku na imeweka kambi katika hoteli ya Bahari Beach, Kunduchi tayari kwa mechi itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa JUmapili hii saa tisa kamili.
Kwa mujibu wa TFF maandalizi yote yamekamilika na mechi hii inatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya watanzania watakaojitokeza uwanjani na kupitia runinga pia.
Ivory Coast inaongoza katika kundi C ikiwa na pointi 10, Tanzania ya tatu na pointi 6, Morocco ya tatu na pointi 5 na Gambia ni ya nne na pointi 1.

Comments