KUELEKEA BRAZIL MWAKANI: TAIFA STARS YAJIWEKA NJIA PANDA

Na Mahmoud Zubeiry, Marrakech,Morocco TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana usiku imefungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Marakech mjini hapa na wenyeji Morocco, Simba wa Atlasi katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani. Stars ilimaliza mechi hiyo pungufu baada ya Aggrey Morris kupewa kadi nyekundu dakika ya 37. Hadi mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Abderazak Hemed Allah baada yay eye mwenyewe kujiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kugongana na Aggrey Morris akatolewa nje. Morocco ndiyo waliocheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza wakishambulia zaidi upande wa kulia alipokuwa akikimbiza Belhanda. Dakika ya 25 Thomas Ulimwengu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki, lakini shuti lake likadakwa na kipa. Kocha Kim Poulsen aliwapumzisha kwa mpigo washambuliaji Mrisho Ngassa na Ulimwengu dakika ya 44 na kuwaingiza beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’. Kipindi cha pili Morocco walirejea na moto tena, wakiishambulia zaidi Stars iliyoonekana kudhoofika na katika dakika ya 50 Youssef El Arabi akafunga bao la pili kiulaini baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania na kubaki na kipa Juma Kaseja. Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza liliipatia Stars bao la kufutia machozi dakika ya 61 lililofungwa na Amri Kiemba kwa shuti la mbali kutoka wingi ya kushoto. Morocco waliendelea kutawala mchezo na Stars walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushitukiza ambayo kwai kiasi fulani yalikuwa ya matumaini. Dakika ya 82 Kim alimpumzisha Vialli na kumuingiza John Bocco ‘Adebayor’ ambaye aliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji. Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast. Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yenye pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao 10 baada ya kuifunga Gambia 3-0 leo. Wiki ijayo Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager watakuwa wenyeji wa Ivory Coast mjini Dar es Salaam Morocco ikimenyana na Gambia. Stars inaweza kufufua matumaini ya kucheza Kombe la Dunia ikiifunga Ivory Coast, kwani kama Tembo watafungwa na mechi ya mwisho na Tanzania ikashinda, itasonga mbele. Stars inaondoka leo asubuhi hapa (juni 9) kwenda Casablanca kuunganisha ndege kurejea Dar es Salaam ikipitia Cairo, Misri, tayari kuanza maandalizi ya kuivaa Ivory Coast. Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Frank Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mchadk44/John Boccodk82, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa/Nadir Haroub dk44.

Comments