KASEJA AMALIZANA KIAINA NA SIMBA SC

WAKATI viongozi wa klabu ya Simba wakivutana juu ya usajili wa kipa wake namba moja, Juma Kaseja (pichani), nyota huyo amelegeza masharti aliyokuwa ametoa ili aendelee kukipiga Msimbazi.
Habari ambazo Sports Lady Blog imezipata zinasema mgawanyiko huo umejitokeza hivi karibuni wakati wa kumjadili Kaseja kwa wengi kutaka aongezewe mkataba kama moja la sharti la nahodha huyo.
Awali, Kaseja alitaka kusainishwa miaka miwili kwa dola 40,000 za Marekani na kuhakikishiwa nafasi yake kama kipa namba moja, masharti ambayo yalipingwa na baadhi ya viongozi hasa wadau.
Kuna habari kuwa baada ya mazungumzo baina ya uongozi na Kaseja wameafikiana kumsainisha mwaka mmoja na dau la
sh milioni 30, suala ambalo litatekelezwa ndani ya siku chache zijazo hasa baada ya mechi ya Juni 16 kati ya Taifa Stars na Ivory Coast.
Siku hiyo Stars iliyopo kambini itawakaribisha Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kundi C, katika kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwakani. 
“Mjadala wa Kaseja tumeshaufunga ingawa hatukuyapa kipaumbele matakwa yake. Tunasubiri amalize jukumu la kuitumikia Stars, tuingie naye mkataba mpya,” kilisema chanzo hicho.

Aidha, Simba imeachana na harakati za kumsajili beki wa kimataifa wa Uganda, Robert Ssenkoom, kwa kutoridhishwa na kiwango chake licha ya kupewa nafasi hiyo tangu atue nchini Juni 4.