IVORY COAST WATUA, TIKETI ZA MECHI YAO NA STARS KUANZA KUUZWA MCHANA WA LEO

Wakati timu ya Ivory Coast ikiwasili nchini jana usiku kwa ndege maalum, tiketi kwa ajili ya mechi kati yake na Taifa Stars itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa zinaanza kuuzwa leo mchana (Juni 14 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
 Vituo vitakavyotumika kwa mauzo hayo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
 Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, sh. 7,000 viti vya rangi ya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
 Pia viti 100 vilivyo katika sehemu ya Wageni Maalumu (VVIP) vitauzwa kwa sh. 50,000 kila kimoja. Tiketi hizo zitauzwa katika ofisi za TFF, na watakaonunua watapewa kadi maalumu zenye majina yao, majina ambayo pia watayakuta katika vita watakavyokaa. Kwa maana hiyo hakutakuwa pasi maalumu (free pass) za kuingia VVIP.