FM ACADEMIA KUPAMBA MISS KIGAMBONI NI JUNI 7@NAVY BEACH

Na Mwandishi Wetu
BENDI ya FM Academia maarufu Ngwasuma wanatarajia kutoa burudani katika shindano la kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni 'Redd's Miss Kigamboni 2013' litakalofanyika Ijumaa Juni 7 kwenye ukumbi wa Navy Beach.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yako katika hatua za mwisho na wanamuziki wa bendi hiyo wameahidi kuonyesha burudani nzuri.
Alisema kuwa Ngwasuma wanatarajia kutumia shindano la Redd's Miss Kigamboni kutambulisha nyimbo zake mbili mpya ziitwazo Chuki ya Nini na mwingine uitwao Fataki.
Aliongeza kuwa warembo wanaendelea na mazoezi katika hatua za mwisho na wameahidi kutoa ushindani kwenye mashindano ya ngazi ya kanda ya Temeke baadaye mwezi ujao.
Alisema kwamba wanawashukuru wadau wote waliojitokeza kudhamini shindano hilo na kuongeza kuwa warembo 13 watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Taji la Redd's Miss Kigamboni linashikiliwa na Edda Sylivester ambaye alishika nafasi ya tatu katika shindano la Miss Tanzania mwaka jana.
Katika kuwaanda washiriki wa shindano hilo, kamati ya Miss Tanzania chini ya Hashim Lundenga na mrembo wa nchi wa mwaka 1999, Hoyce Temu, walitembelea kambi hiyo ili kuwafunda warembo wawe tayari na uelewa wa sanaa ya urembo.
Mwisho.