SOFAPAKA YAJA KUWAANIKA NYOTA WAPYA WALIOSAJILIWA SIMBA NA YANGA


NYOTA wapya waliosajiliwa katika klabu kongwe za Simba na Yanga wanatarajiwa kuanza kuonekana kwenye mechi za kirafiki baina ya timu hizo na timu ya Sofapaka ya Kenya,imefahamika.
 Mratibu wa ziara hiyo George Wakuganda alisema jana kwamba maandalizi ya ujio wa Sofapaka yanaendelea vema ambapo timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini Juni 10 mwaka huu. 
Alisema lengo la ujio wa timu hiyo ni kuzipa makali Simba na Yanga kabla ya kwenda kushiriki kwenye michuano ya klabu bingwa Afika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame itakayofanyika kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 mwaka huu nchini Sudan. 
Alisema ikiwa nchini Sofapaka itakwaana na Simba Juni 12 kabla ya kukipiga na Yanga juni 13 ambapo mechi zote zitafanyika kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. 
Tayari Simba imeanza mazoezi jana kwenye uwanja wa Kinesi, huku Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara na watetezi wa michuano ya Kagame wakitarajiwa kuanza kujinoa Juni 3 mwaka huu.