RAIS KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA MDHAMINI WA SIMBA MZEE ALLY KLEIST SYKES LEO

 Marehemu Mzee Ally Kleist Sykes
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilali, Rais wastaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Mzee Benjamin William Mkapa, Waziri Mkuu Mstaafu Dkt Salim Ahmed Salim, Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kianana wakiungana na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya Mzee Ally Kleist Sykes, mmoja wa waasisi wa chama cha TANU, leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam leo Mei 20, 2013

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimfariji mjane wa marehemu Ally Sykes, Zainab Ally, wakati alipofika kuhani msiba huo wa mwasisi wa TANU, aliyefariki jana jijini Nairobi. Marehemu Sykes anazikwa leo jioni jijini Dar es Salaam. Picha na OMR


MWENYEKITI wa klabu ya soka ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage (Mb), kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya Simba, Wapenzi na Wanachama wa klabu anapenda kutoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu. jamaa na marafiki wa aliyekuwa mdhamini wa Simba, Mzee Ally Kleist Sykes (86) aliyefariki dunia juzi jijini Nairobi, Kenya.
Mzee Sykes, mmoja wa wadhamini wa muda mrefu wa Simba, alikwenda Nairobi kwa matibabu na Rage amesema msiba huu ni pigo kubwa sana kwa klabu.
"Kwa watu ambao wameifahamu Simba kwa muda mrefu, watafahamu namna Mzee Sykes alivyokuwa msaada mkubwa wa hali na mali kwa klabu. Tangu mambo ya wafadhili hayajaanza, yeye alikuwa baadhi ya watu waliokuwa wakiisaidia Simba kwa moyo wao wote. Aliteuliwa kuwa mdhaamini kutokana na busara zake, mapenzi yake kwa klabu na uadilifu aliokuwa nao," alisema Rage.
Ally Kleist Sykes alizaliwa mnamo Septemba 10, mwaka 1926 jijini Dar es Salaam. Alikuwa miongoni mwa watoto watatu wa kiume wa Mzee Kleist Sykes; miongoni mwa waasisi wa chama cha TAA ambacho baadaye kilikuja kujulikana kama TANU kilicholeta uhuru wa Tanganyika (TANZANIA). Kaka zake wengine ni Abdul Wahid (marehemu) na Abbas.

Kutokana na msiba huo, Rage amesema Simba inatoa ubani wa kiasi cha Sh milioni moja.

Majina ya akina Sykes hayana asili ya kawaida ya majina ya kibantu kwa vile walikuwa na asili ya kabila la Wazulu kutoka Afrika Kusini.

Mzee Sykes anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar ambapo marehemu baba na kaka yake walizikwa.

Imetolewa na

Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

Comments