Msanii mahiri wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu kama
Mwana FA ambae ni Balozi wa Chapa Vodacom amesema hadhi na heshima ya mwanaume
katika jamii itakuwa na uzito mbele ya
uso wa jamii kwa wao kuwa tayari kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii
na wala si vinginevyo.
Balozi huyo maarufu kwa jina la Mwana FA ametoa kauli hiyo
mjini Dodoma wakati wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu fistula iliyofanyika
katika viwanja vya Nyerere Square kuelekea siku ya fistula dunaini Mei 23.
Kampeni hiyo inadhaminiwa na kampuni ya Vodacom na Vodafone ya Uingereza
ikiihusisha mikoa mbalimbali.
Balozi huyo amesema ni wazi kwamba wanaume wamekuwa wamiliki
wa maamuzi katika jamii huku wakitajwa kuwa nguzo ya familia lakini sifa hizo
na mamlaka hayo yatakuwa na dosari kubwa iwapo hawatokuwa pia mstari wa mbele
katika kuhakikisha jamii inapata suluhisho la matatizo.
Balozi huyo ambae alikuwa akielimisha wakazi wa mji wa
Dodoma kuhusu fistula, amesema fistula sio tatizo kama ambavyo inaweza
kufikiriwa kwa kuwa jambo gumu lingekuwa namna ya kupata matibabu na uwezo wa
kugharamia matibabu hayo.
“Hakuna mwanamke ambaye anapata fistula bila ya mwanaume
kuwa chanzo kwa kuwa ndio tunaowapa ujauzito wake zetu, hivyo sio vema na haki
kwa mwanaume kumkimbia mkewe au kumtenga mwanamke eti tu kwa sababu mwanamke
huyo ana tatizo la fistula.”Alisema Balozi huyo
“Nawaomba sana wakazi
wa Dodoma hasa wanaume tubadili mtazamo tulinao juu ya fistula kwa kutambua
kwamba sisi ndio chanzo cha wanawake kupata fistula lakini zaidi ni kwamba hilo
sio tatizo kwa kuwa tatizo ni lile ambalo halina suluhisho, fistula inatibika
na tena inatibika bila malipo kwa ufadhili wa Vodacom na Vodafone, nini zaidi
tunachohitaji katika hili?.”Alihoji Mwana FA
Amesema uamuzi alioufanya kukubali kutembea nchi nzima
kuhamasisha akina baba kuondokana na dhana hasi juu ya fistula ikiwemo
kuhusisha tatizo hilo na ushirikina au laana na hivyo kuwakimbia wake zao au
kushiriki kwa namna yoyote katika kuwanyanyapaa wanawake wenye tatizo la
fistula ulikuwa ni mgumu lakini alikubali kwa kuwa anaamini jamii itamuelewa.
“Haikuwa kazi rahisi kwangu kukubali kuongoza msafara huu
lakini baada ya kutathmini na kuona jinsi akina mama wanavyoteseka kwa tatizo
hili nilijihisi mwepesi kukubali kuzunguka kila kona kuongea na wanaume
wenzangu kuwahamasisha kuwa tayari kwa pamoja kuunga mkono kampeni hii ili
kufikia lengo la Vodacom la kumaliza tatizo la fistula ifikapo mwaka 2016
.”Aliongeza
“Iwapo kuna mtu(Vodacom)amejitolea kutoa suluhisho la tatizo
kwa kulipia nauli, chakula, malazi na matibabu hatuwezi tena kusema fistula ni
tatizo,kikwazo pekee tulichonayo hapa ni kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na
taarifa na ujumbe huu.”Aliongeza
Mwana FA amekuwa chachu katika kampeni hii kwa namna ambavyo
ushawishi wake umewezesha kwa kiasi kikubwa ujumbe wa fistula kuwaingia wanaume
huku baadhi yao wakimuahidi kumuunga mkono kwa dhati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto Ummy Mwalimu alisema si haki kuendelea kuwaacha wanawake wakiteseka
wakati fursa ya kuwawezesha kupata matibabu ipo na hivyo ameitaka jamii kuiunga
mkono kampeni hiyo na kuitumia ipasavyo.
“Tunaishukuru Vodacom kwa kuweka mfumo wezeshi kwa jamii
kupata elimu ya fistula na pia kuwawezesha wanawake kupata matibabu ya fistula
bila malipo, naomba wakazi wa mji wa Dodoma na nchi nzima tuitumie fursa hii na
tuwe mabalozi kwa wenzetu.”
“Vodacom inafanya kazi kubwa sana kusaidia jamii hapa
nchini. Kamwe hatutoona aibu kuipongeza ndani na nje ya Bunge kwa kazi hiyo
kubwa na znuri wanayoifanya ikiwemo kampeni hii ya fistula na ufadhili inaotoa
kwa wanawake kupata matibabu bila malipo.”Alongeza Ummy
Amesema kuwa jamii lazima ione na kutambua kuwa mwanamke ana
wajibu wa kuwa na afya njema ili nae aweze kushiriki katika shughuli za kijamii
na za kiuchumi na hivyo kuchangia maendeleo ya kaya na jamii anamoishi.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwepo kwa hali ya unyanyapaa kwa
jamii kwa wanawake wanaokabiliwa na matatizo ya fistula hali ambayo amesema ni
lazima ibadilike hasa wakati huu ambapo fursa za matibabu bila malipo zipo
ikiwepo na kuahidi kuibeba ajenda hiyo kwa nguvu zake zote.
Vodacom hutumia wastani wa Sh 700,000 hadi 900,000 kulipia
matibabu ya mgonjwa mmoja wa fistula kwenye hospitali ya CCBRT.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii Said Mtanda amesema anatambua vema tatizo la fistula na athari zake kwa
wanawake wazazi na kwamba pamoja na ukweli kuwa amekuwa akichukua juhudi
binafsi katika kusaidia wanawake wenye fistula lakini sasa anaibeba kampeni
hiyo na kuiwasilisha katika kamati yake ili kuipa nguvu rasmi za kibunge.
“Naahidi kuwa nitawasilsiha kwenye kamati yangu ujumbe wa
kamati hii ikiwa ni pamoja na kuiomba nguvu za kamati hiyo na kuwashawishi
wajumbe kuubeba ujumbe wa kampeni hii ndani ya Bunge ikiwemo wakati wa shughuli
rasmi za kamati na Bunge kwa ujumla.”Alisema Mtanda
Kampeni hiyo iliyolenga kuifikia mikoa mbalimbali itamaliza
safari yake Mei 23 jijini Dar es salaam siku ya fistula Duniani.
Comments
Post a Comment