MISS KIGAMBONI KUSAKWA JUNI 7@NAVY BEACH

Na Mwandishi Wetu
SHINDANO la kumtafuta mrembo wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" linatarajiwa kufanyika Ijumaa Juni 8 kwenye ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 2:00 usiku hapa jijini Dar es Salaam.
Tayari warembo wameshaanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na shindano hilo ambapo wanajifua kwenye ukumbi wa Break Point (VIP) uliopo Posta hapa jijini.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yako katika hatua za mwisho na bado wanakaribisha warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo kufika mazoezini kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Mratibu huyo alisema kwamba lengo la kuweka wazi na kuwahamasisha warembo ni kutaka kutoa nafasi kwa wasichana wengi zaidi kujiandikisha na hatimaye kupata mshindi atakayekiwakilisha vyema kitongoji hicho katika mashindano ya ngazi ya Kanda yatakayofanyika baadaye mwezi ujao.
"Tumeshaanza maandalizi na tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo wa hapa nchini kujiandaa kusubiri Kigamboni kutoa mrembo wa taifa mwaka huu, tunawashiriki wenye mvuto na sifa za ushindani," alisema Somoe.
Aliongeza kwamba fomu kwa ajili ya kushiriki shindano hilo zinapatikana bure na warembo wanafanya mazoezi chini ya Blessing Ngowi, ambaye mwaka juzi alishiriki fainali za taifa za Redd's Miss Tanzania na alitwaa taji la Kanda ya Elimu ya Juu.
Alisema pia makampuni na taasisi mbalimbali zinakaribishwa kudhamini shindano hilo ambalo mwaka jana lilitoa mshindi katika kinyang'anyiro cha Kanda ya Temeke ambaye ni Edda Sylivester.
Edda alifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za taifa huku mshindi wa taifa ni Brigitte Alfred ambaye mwaka huu ataenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya dunia.