MISS KIGAMBONI KUANZA KUJINOA J'3 @BREAK POINT

Na Mwandishi Wetu
MAZOEZI kwa ajili ya kujiandaa na shindano la kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" yanatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Jumatatu Mie 6 mwaka huu kwenye ukumbi wa Break Point uliopo Posta jijini Dar es Salaam.
 Mratibu wa shindano hilo, wa kampuni ya K& L Media Solutions, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yanaendelea na bado nafasi iko wazi kwa wasichana wote wenye sifa za kushiriki shindano hilo kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Mratibu huyo alisema kwamba lengo la kuweka wazi na kuwahamasisha warembo ni kutaka kutoa nafasi kwa wasichana wengi zaidi kujiandikisha na hatimaye kupata mshindi atakayekiwakilisha vyema kitongoji hicho katika mashindano ya ngazi ya Kanda yatakayofanyika baadaye mwezi ujao.
"Kila kitu kinaendelea vizuri na kamati ya maandalizi imewataka wadau wa sanaa ya urembo kujiandaa kuona mwaka huu shindano likiwa lenye ubora na mvuto," alisema Somoe.
Aliongeza kwamba fomu kwa ajili ya kushiriki shindano hilo zinapatikana bure na washiriki ambao wako tayari wanaombwa kufika siku ya Jumatatu ili kuanza mazoezi.
Alisema pia makampuni na taasisi mbalimbali zinakaribishwa kudhamini shindano hilo ambalo mwaka jana lilitoa mshindi katika kinyang'anyiro cha Kanda ya Temeke ambaye ni Edda Sylivester.
Edda alifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za taifa huku mshindi wa taifa ni Brigitte Alfred ambaye mwaka huu ataenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya dunia.