KILIMANJARO PREMIUM LAGER YAIZAWADIA YANGA MIL.25

Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh. Mil. 25 kwa Katibu Mkuu wa Yanga,Laurance Mwalusako kama zawadi ya ubingwa wa Ligi Kuu.Wanaoshuhudia ni  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga,Mussa Katabaro (wa pili kutoka kulia) ,Mkurugenzi wa Fedha Yanga,Denis Oundo pamoja na Geoffrey Makau (wa pili kutoka kushoto).

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Lager  imewazadiwa sh milioni 25 mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu ya soka Yanga. 
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Meneja wa kinywaji cha Kilimanjaro, George Kavishe alisema kwamba zawadi hiyo ni sehemu ya ahadi ya udhamini wao kwa timu itakayoshinda ama kushika nafasi za juu. 
Kama wadhamini wa klabu kongwe za yanga na Simba tuliahidi kutoa mil 25 timu itakayotwaa ubingwa wa Ligi kuu n ash mil 15 kwa timu itakayoshika nafasi ya pili, hivyo kutokana na Yanga kutwaa ubingwa ndio tunaikabidhi fedha hizi,”alisema. 
Kavishe aliongeza zawadi hiyo ni sehemu sh bilioni 1.5 ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi zaidi na kusaidia klabu katika maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. 
“na tulifanya hivi makusudi ili  kuleta ushindani kwa timu hizi za Simba na Yanga  ili ziweze kufanya vema kwenye ligi hiyo ambayo imekuwa na ushindani mkubwa. 
“Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa ligi kuu na hivyo kuibuka washindi.Napenda kuwapongeza wachezaji, kocha na uongozi mzima wa Yanga kwa matokeo mazuri ya kushinda ligi kuu kwa mara ya 24 sasa,”alisema. 
Akipokea hundi hiyo,Katibu Mkuu wa Yanga,Lawrance Mwalusako,  pamoja na kushukuru alisema Yanga ni timu nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi imara pamoja na udhamini wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager. 
“mafanikio yetu ya uwanjani ni ikielelezo cha mafanikio pia ya bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla ambayo imekuwa ikitusaidia sana.Bia hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea mafanikio haya,”alisema. 
Mwalusako aliongeza kuwa, Yanga kwa sasa ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la kimataifa la soka kutokana na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager hivyo itaendelea kukua na kufanikiwa. 
Kwa ubingwa huko Yanga itaiwakilisha Tanzania kwenye ligi ya mabingwa Afrika mwakani, pamoja na michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia juni 18 hadi Julai 2 huko Sudan Kusini ambapo Yanga ni mabingwa watetezi. 

Mbali na zawadi hiyo ya TBL, Yanga inatarajiwa kupata kitita cha sh milioni 70 kutoka kwa wadhamini wakuu wa Ligi hiyo, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.