HOMA YA PAMBANO LA WATANI:YANGA WABAKI DAR, SIMBA WAENDA ZENJI

HOMA ya pambano la watani wa jadi nchini Simba na Yanga imezidi kupanda ambapo sasa timu hizo zimeamua kuingia kambini kwa ajili ya hukiandaa na mechi hiyo ya ligi kuu bara itakayopigwa Mei 18 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Ni kawaida kwa timu hizo zinapokjaribia kukwaana kuingia mafichoni, lakini Yanga ambayo tayari imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo imedai haina mpango wa kwenda mafichoni na kesho Ijumaa wachezaji wake wataingia kambini kwenye hosteli za klabu hiyo zilizopo mtaa wa jangwani.
Ofisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto amesema leo kwamba mechi yao ya Simba ni ya kawaida sana hivyo hawana sababu ya kwenda kujichimbia mahali na kuongeza kuwa kikosi kipo kamili na lazima waibuke na ushindi siku hiyo.
Kwa upande wa Simba ambayo imevuliwa ubingwa, kikosi chake kitaondoka kesho kwenda Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.
Simba inayonolewa na Mfaransa Patrick Liewig kupitia kwa kocha wake msaidizi Jamhuri Kihwelo 'Julio' imeweka wazi kwamba siku hiyo ni lazima wakimwagie mchanga kitumbua cha Yanga ili kutibua furaha zao za ubingwa.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.