BREAKING NEWS; YANGA WATUA PEMBA KUWEKA KAMBI YA KULIPA 5-0 MEI 18 TAIFA

Yanga SC

Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 10, 2013 SAA 10:45

KIKOSI cha Yanga SC kimewasili kisiwani Pemba saa moja iliyopita kuweka kambi ya kujiandaa na mpambano dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC Mei 18, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wameondoka kwa siri kubwa leo Dar es Salaam kwa ndege maalum ya kukodi, kwenda visiwani humo kujiandaa na pambano hilo la marudiano la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
BIN ZUBEIRY inafahamu Yanga imefikia katika hoteli ya Samail Morden, mkabala na benki ya PBZ na kesho itaanza mazoezi kwenye Uwanja wa Gombani.
Yanga itakuwa huko hadi siku moja kabla ya mechi itakaporejea Dar es Salaam na kufikia katika hoteli moja kubwa Jijini, kabla ya kuamkia kwenye mechi siku inayofuata.
Pamoja na kwamba Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, lakini inaipa uzito mkubwa mechi hiyo kwa sababu inataka kulipa kisasi cha kufungwa 5-0 na wapinzani wao hao wa jadi mwaka jana.
Tangu umeingia madarakani, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Mehboob Manji umekuwa ukiumia kichwa na kipigo cha 5-0 mwaka jana.
Mara kadhaa Manji amewahi kukaririwa na BIN ZUBEIRY akisema kwamba 5-0 zinamuumiza kichwa hasa katika wakati ambao idadi ya mabao katika mechi za timu hiyo ilipungua.
Wakati Yanga wametua Pemba, kuna wasiwasi Simba SC ikaachana na utamaduni wake wa kuweka kambi Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya wapinzani wao hao.
Kihistoria, Simba SC imewahi kuipa Yanga vipigo viwili vitakatifu 6-0 mwaka 1977 na 5-0 mwaka jana, wakati Yanga iliifunga SImba 5-0 mwaka 1969.  
Safari hii, Yanga imepanga kuweka heshima kwa kuhakikisha inaipa kipigo kitakatifu Simba cha kuvunja rekodi ya 6-0.