AZAM FC YAFA KIUME MOROCCO, YAPIGWA 2-1


Kipa wa AS FAr Rabat, Ali Grouni akimfariji mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco baada ya kukosa penalti ambayo ineipa Azam tiketi ya kufuzu Kombe la Shiriksiho jioni hii kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Rabat. Azam imefungwa 2-1. 

Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
SOKA ni mchezo wa bahati wakati mwingine. Naam sadakta, usemi huo umedhihirika leo kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah baada ya Azam kulala 2-1 mbele ya wenyeji AS FAR Rabat na kutolewa katika Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya kupata nafasi nzuri ya kusonga mbele dakika ya 81.
“Tumekosa penalti dakika ya 81, siwezi kumlaumu refa ikiwa tumekosa penalti zimebaki dakika tisa,” alisema kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall baada ya mchezo akizungumza na BIN ZUBEIRY.
Azam ilihitaji sare yoyote ya mabao ifuzu na ilikaribia kuipata dakika ya 81 ilipopata penalti ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini fundi wa upigaji wa michomo hiyo, John Raphael Bocco alikwenda kugongesha mwamba mpira huo.
Dakika ya 88, kona nzuri iliyochongwa na Khamis Mcha ‘Vialli’ iliunganishwa vizuri kwa kichwa na Bocco, lakini beki mmoja wa Rabat akaiwahi kwenye chaki na kuiondosha kwenye eneo la hatari.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Abib Charef Medh aliyesaidiwa na Mahmoud Bitam na Mohamed Mekous wote kutoka Algeria, hadi mapumziko, Rabat walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya sita, mfungaji John Raphael Bocco kwa mpira wa adhabu, baada ya beki mmoja wa Rabat kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Boko alipiga shuti zuri ambalo liliupita ukuta wa Rabat na kumpoteza maboya kipa wao, Ali Grouni na kutinga nyavuni.
Mashabiki wa Rabat walianzisha fujo baada ya bao hilo na kujikuta wakipambana na Polisi. Idadi ya Polisi iliongezwa uwanjani ili kuwadhibiti mashabiki hao ambao walikuwa wakivunja viti na kuwatupia Polisi.
Iliwachukua dakika sita tu Rabat kusawazisha kupitia kwa Abdelrahim Achchakir kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki David Mwantika kumchezea rafu mchezaji wa Rabat.
Refa Abib Charef Medh alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Achchakir kwa kumchezea rafu Brian Umony dakika ya 35.
Hata hivyo, Azam walishindwa kutumia mwanya wa Rabat kucheza pungufu na kujikuta wakifungwa wao bao la pili.
Mustafa Allaoui alipiga vizuri shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita 25 na kumtungua Mwadini Ally dakika ya 42.
Baada ya bao hilo, wenyeji waliendelea kulisakama kama nyuki lango la Azam licha ya kucheza pungufu.
Viungo wa Azam walionekana kabisa kuzidiwa na viungo wa Rabat ambao waliifanya timu hiyo itawale mchezo. Azam haikufanya shambulizi la kushitua tangu wafungwe bao la pili.
Kipindi cha pili, mchezo ulizidi kuwa wa kasi na mashambulizi ya panede zote mbili, lakini kilianza vibaya kwa Azam, baada ya beki wake David Mwantika kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 56 kwa kumchezea rafu mchezaji wa Rabat.
Mwantika leo hakuwa katika ubora wake- kwani hata faulo alizocheza na kusababisha penalti ilikuwa ‘si ya lazima’ na hata kadi nyekundu pia angeweza kuiepuka kama asingemsukuma hadi kwenye lami mchezaji wa Rabat.  
Kutokana na Azam kubaki pungufu, Rabat walizidisha mashambulizi langoni mwa wageni na Kaddioui Yuossef alikuwa mwiba kwa timu ya Stewart.
Waziri Salum alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kumchezea rafu Kaddioiu Yuossef.
Ajabu baada ya kadi hiyo, Azam walizinduka na kuanza kulishambulia kama nyuki lango la Rabat na ndipo dakika ya 81 beki mmoja wa Rabat alipounawa mpira kwenye eneo la hatari na refa akamuru penalti ambayo Bocco alikosa.
Wakati mashabiki wachache wa Tanzania waliokuwa uwanjani wakishangilia kwa kuamini Bocco anafunga, aligongesha mwamba mpira na kuinyima nafasi muhimu Azam.    
Baada ya mchezo huo, kocha Stewart alisema kwamba wamefungwa kwa sababu ya makosa ya safu ya ulinzi. “Kweli refa alikuwa wa upande mmoja, bao la pili (la Rabat) halikuwa sahihi, aliotea. Kadi ya Waziri haikuwa sahihi, walikuwa wanapambana (wachezaji), lakini bado siwezi kumlaumu ikiwa aliipa timu yangu penalti zimebaki dakika tisa,”alisema.
Azam sasa imetolewa kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya awali wiki mbili zilizopita kutoka sare ya bila kufungana Dar es Salaam na Waarabu hao.
Rabat sasa watamenyana na moja ya timu zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa kusaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shikrikisho.
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco, Humprey Mieno/Gaudence Mwaikimba dk79  na Brian Umony/Khamis Mcha dk70.
AS FAR Rabat; Ali Grouni, Anouar Younes/Ennajar Tarik, Younes Hammal, Younes Belakhdar, Kaddoui Youssef, Abdelrahim Achchakir, Aqqal Salaheddine/Alloudi Soufiane, Mustafa Allaoui, El Kodry Yassine, El Bakkali Medamine na El Yousfi Mostafa.

Comments