Na Prince Akbar, Tanga
YANGA bingwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2012/2013.
Habari ndiyo hiyo. Yanga ya Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu jioni
hii, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo baina ya wenyeji Coastal
Union na Azam FC ya Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Matokeo hayo yanamaanisha, Azam FC waliokuwa washindani
wakuu wa Yanga SC yenye pointi 56, hawawezi tena kufikisha pointi hizo ambazo
wanazo mabingwa hao wapya, kwani hata wakishinda mechi zao nyingine mbili zilizobaki, watamaliza na pointi 54.
Mchezaji aliyepeleka shangwe na vigelegele Jangwani leo ni
Danny Lyanga, ambaye aliifungia Coastal bao la kusawazisha dakika ya 72.
Lyanga ambaye ilibaki kidogo asajiliwe Yanga msimu huu
kutoka Toto Africans, kama si kuzidiwa kete na Coastal, alifunga bao hilo
katika mpira wake wa kwanza kuugusa tangu aingie kuchukua nafasi ya Suleiman
Kassim ‘Selembe’ dakika ya 71.
Alifunga bao hilo, baada ya kupokea pasi nzuri ya
mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Pius Kisambale, ambaye ni mdogo wa kiungo
wa Wana Jangwani hao, Athumani Iddi ‘Chuji’.
Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo wa
leo, lililofungwa na beki Aggrey Morris kwa penalti dakika ya 60, baada ya
mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Gaudence Mwaikimba kuchezewa rafu kwenye
eneo la hatari na beki Yussuf Chuma- na
refa Andrew Shamba wa Pwani akaamuru pigo hilo.
Baada ya bao hilo, Coastal walionekana kufanya jitihada za
wazi kusawazisha na ndipo Lyanga aliyetokea benchi akawapa ubingwa Yanga.
Matokeo haya yanakuwa sawa na Coastal kulipa fadhila kwa
Yanga, kwani hata wao, ubingwa wao pekee wa Ligi Kuu waliochukua mwaka 1988
ulitokana na ‘msaada’ wa wana Jangwani huo.
Msimu huo, mshindani wa Coastal katika mbio za ubingwa
alikuwa Simba SC ambaye ili kutwaa taji hilo, alihitaji kushinda mechi ya
mwisho dhidi ya African Sports mjini Tanga huku akiomba Wagosi wa Kaya walale
mbele ya Yanga Uwanja wa Taifa.
Lakini Yanga wakacheza ‘kichovu’ na Athumani China akaenda
kupiga penalti ‘kiviivu’ akakosa, Coastal ikishinda 2-0 na kusherehekea taji
pekee la ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya Simba pia kushinda 3-0 dhidi ya Sports
Tanga.
Hili linakuwa taji la 24 kwa Yanga, tangu watwae kwa mara ya
kwanza mwaka 1968.
Aidha, huu unakuwa msimu wa pili mfululizo, Azam
wanaukosakosa ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya msimu uliopita pia kuzidiwa kete na
Simba SC.
CHANZO:bongostaz blog
Comments
Post a Comment