Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea katika raundi yake ya
25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam,
Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL
msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya washabiki
wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa
kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati
mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi
hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni
sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya
chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi
zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi
namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja
wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika
nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na
wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu
na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake
Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.
Comments
Post a Comment