TFF YAWAPA SOMO NYOTA WA TANZANIA


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa wito kwa wachezaji wa Tanzania wanaoziwakilisha klabu zao kwenye michuano ya kimataifa, kuonesha nidhamu nzuri uwanjani ili kuepuka adhabu ya kadi nyekundu.
Hatua hiyo inatokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutoa kanuni mpya, ambapo mchezaji atakayepata adhabu ya kadi nyekundu ataitumikia pia katika timu yake ya taifa.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba kwa hali hiyo, wachezaji hawana budi kuwa makini wawapo uwanjani, kwani adhabu hiyo itakuwa ni hasara kwa taifa pia.
Alisema ni muhimu kwa wachezaji wa timu husika kucheza kwa kufuata sheria 17 za soka ili kuepukana na adhabu hiyo itakayomfanya ashindwe kuitumikia pia timu ya Taifa.