TFF YABARIKI AZAM FC KWENDA TAKUKURU


SIKU chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kutowaona na kesi ya kujibu nyota wanne wa Azam FC, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kitendo cha uongozi wa klabu hiyo kulifikisha suala hilo katika taasisi hiyo kilikuwa sahihi.
Azam iliwafikisha Takukuru wachezaji wake, Deogratius Munishi ‘Dida’, Aggrey Morris, Said Mourad na Erasto Nyoni kwa madai ya kupokea rushwa ya sh milioni saba kutoka klabu ya Simba ili wacheze chini ya kiwango.
Kitendo hicho kimekuwa kikikosolewa na wadau mbalimbali wa soka, kwa madai uongozi wa Azam FC ulikuwa na uwezo wa kulishughulikia na hata kulifikisha katika vyombo vya kinidhamu vya TFF.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba Takukuru ndiyo taasisi pekee inayoshughulikia masuala ya rushwa nchini, hivyo Azam hawakukosea kwenda huko.
“Masuala yote yanayohusu rushwa, hata katika michezo, Takukuru ndiyo inahusika nayo, hivyo Azam FC ilikwenda kule kwa mujibu wa taratibu zinazostahili,” alisema.
Kuhusiana na sakata hilo, ambalo nyota hao watuhumiwa walilifikisha Kamati ya Katiba, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Osiah alisema wachezaji wenyewe wataamua kama watataka liendelee kuchunguzwa ama la.
Tayari uongozi wa Simba, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage, umedai kwenda mahakamani kuidai Azam fidia ya sh bilioni 1.8 na kuombwa radhi, kwa madai ya kuchafuliwa kutokana na tuhuma hizo.

Comments