SIMBA YAWAPA MAPUMZIKO WACHEZAJI WAKEMARA baada ya mechi ya jana dhidi ya Azam FC, wachezaji wote wa Simba walipewa mapumziko ya siku mbili (leo na kesho) na timu itaanza tena mazoezi keshokutwa Jumatano asubuhi katika viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wamepewa mapumziko hayo kutokana na kutumika kwa kipindi kirefu mfululizo tangu timu ilipokwenda katika mikoa ya kanda ya ziwa na kambini Bamba Beach jijini Dar es Salaam.
Ni matarajio ya uongozi na benchi la ufundi kwamba wachezaji hao wataanza mazoezi wakiwa na nguvu mpya na tayari kwa changamoto ya mechi nne zilizobaki kumalizia Ligi Kuu ya Tanzania.
Uongozi wa Simba unawaomba wapenzi na wanachama wake kuendelea kuisapoti timu yao kwa namna ileile waliyoionyesha katika mikoa ya kanda ya ziwa na dhidi ya Azam jana. Ingawa uwezekano wa kutwaa ubingwa haupo wala kutwaa nafasi ya pili, lakini bado kuna kazi ya kutetea heshima na hadhi ya Simba ili iweze kumaliza katika nafasi nzuri.
Wachezaji na viongozi hawataweza kufanya lolote pasipo umoja na mshikamano wa wapenzi na wanachama wake. Kama kauli mbiu ya Simba isemavyo, “NGUVU MOJA.”