SIMBA YAKANA 'USHKAJI' NA YANGA, MECHI YAO NA AZAM YAINGIZA MIL.66

 

KUNA ujumbe mfupi wa maneno umeenezwa kwenye baadhi ya simu za mkononi za wapenzi wa Simba zikidai kwamba washabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia klabu yetu jana walifanya hivyo kwa sababu klabu hizi mbili zimeingia katika mahusiano.
Ujumbe huo ukadai kwamba lengo la mahusiano hayo mapya baina ya Simba na Yanga ni kuhakikisha kwamba Simba inafungwa kwa idadi kubwa ya mabao kwenye mechi ya watani wa jadi Mei 18 mwaka huu.
Ujumbe huo, ukaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hata kambi ya Simba ya Bamba Beach imefadhiliwa na Yanga.
Ujumbe huo wa simu ni wa kuchekesha. Na unachekesha sana. Yeyote aliyetunga meseji hii ana nia ya kuleta machafuko ndani ya klabu ya Simba. Inaonekana haridhishwi na hali ya amani iliyopo klabuni kwa sasa.
Uongozi wa Simba unakana kuwepo kwa mahusiano yoyote ya kuhujumu timu baina ya viongozi wa klabu na Yanga. Kitendo cha kushangiliwa kwa timu pinzani si kigeni kwani kimewahi pia kutokea katika nchi kadhaa duniani.
Ikumbukwe kwamba kimsingi, si jinai au mwiko kwa shabiki wa Yanga kuishangilia Simba. Kama washabiki wa wapinzani wetu wa jadi walivutiwa na kiwango chetu na kuamua kutushangilia, hiyo haikuwa dhambi.
Uongozi unapenda kuwaomba wanachama wa Simba kuwa na imani na uongozi wao na kufahamu kwamba unafanya kila unaloweza kulinda na kuhifadhi hadhi na heshima ya klabu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Simba iliyochezwa jana (Aprili 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 66,855,000 kutokana na watazamaji 11,458.

Viingilio katika mechi hiyo namba 155 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,587,177.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,198,220.34.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,925,683.45, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 4,755,410.07, Kamati ya Ligi sh. 4,755,410.07, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,377,705.03 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,849,326.14.

Comments