SIMBA SC WALIA MECHI YAO NA RUVU SHOOTING KUPIGWA KALENDA


Adobe Systems SIMBA SPORTS CLUB      
P.O.BOX 15318 | TEL+255 222183330 |FAX +255 222183330 |MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET | DAR ES SALAAM | TANZANIA | EMAIL   simbasportsclub@yahoo.com|WEBSITE www.simba.co.tz| AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA
                                                                                       25/04/2013
                    TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UONGOZI wa Simba umekubaliana na hatua ya serikali kuzuia kuchezwa kwa mchezo uliopangwa kuchezwa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania baina ya Wekundu wa Msimbazi na Ruvu Shooting Stars.
Hata hivyo, uongozi wa Simba haujafurahishwa na namna uzuiaji huo ulivyofanyika. Taarifa imetolewa leo kwenye siku ya mechi yenyewe wakati maandalizi yote yakiwa yamefanyika na hivyo kusababisha matatizo katika sehemu kubwa tatu.
Mosi, uongozi wa Simba umeingia gharama kubwa ya kuweka timu kambini na kujiandaa na mechi. Pili, benchi la ufundi na wachezaji walikuwa tayari wamejiandaa na mechi kimwili na kiakili na kuahirishwa huku kwa mechi kumesaidia tu kuvuruga programu. Tatu, wapenzi na washabiki wa Simba wamepata usumbufu wa kwenda uwanjani na kukuta hakuna mechi.
Uongozi wa Simba unapenda kutumia nafasi hii, katika namna ya kipekee kabisa, kuwaomba radhi wapenzi na wanachama wake ambao walifika Uwanja wa Taifa kutazama mechi ambayo haikuwapo.
Washabiki ndiyo wanaoifanya Simba na mchezo wa mpira wa miguu nchini uwe na umaarufu ulionao na bila wao ligi yetu inaweza kupoteza nguvu na ushindani ilionao.
Simba SC inapenda kuwe na utaratibu unaojulikana wa kuahirisha mechi wa walau saa 48 kabla ya siku ya mechi. Hii itasaidia pande zote zinazohusika. Kama mechi imeshindikana kwa sababu za nje ya uwezo wa kibinadamau (Force de Majeure) kama vile mafuriko, tetemeko la ardhi na vimbunga, mechi inaweza kuahirishwa ghafla lakini si kwa mechi ambayo uwepo wake ulifahamika miezi kadhaa nyuma.
Tunashauri pia kwamba siku za mechi ambapo Ligi Kuu inachezwa (match days), inatakiwa kuwa zinafahamika na isiwe kila siku mechi zinachezwa. Simba ilikuwa na mechi wikiendi iliyopita na Ruvu ilikuwa na mechi Mbeya zaidi ya wiki moja iliyopita na hivyo mechi hii ingeweza kuchezwa hata jana (Jumatano) ambayo ni siku ya kawaida kwa mechi kuchezwa badala ya leo Alhamisi.
Ni matumaini yetu kwamba kuahirishwa kwa mechi hii kutakuwa fundisho kubwa katika upangaji wa ratiba na uahirishaji wa mechi ambao una faida kwa pande zote husika.