MAPATO UWANJA WA TAIFA AIBU TUPU


Martin Malera, Dodoma

SERIKALI imeambulia sh bilioni 1.5 ya mapato yanayotokana na michezo ya soka na shughuli nyingine zinazofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar Salaam. 
Serikali imepata kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha miaka saba kutoka mwaka 2007 hadi Februari mwaka huu. 
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Philipa Mturano (CCM), Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, alisema mapato hayo yametokana na mgawo wa asilimia 15 wa kila mechi na shughuli zinazofanyika kama ada ya matumizi ya uwanja. 
Akizungumzia namna Halmashauri ya Manispaa Temeke inavyofaidika na mapato hayo, Makalla alisema mapato ya tozo la ada ya asilimia 15 huingizwa kwenye mfuko wa Serikali Kuu. 
Alisema mapato hayo hutumiwa na serikali katika kutoa huduma kwa Watanzania wote pamoja na Manispaa ya Temeke. 
Aliongeza kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke hunufaika zaidi, kwani matukio yote yanayofanyika Uwanja wa Taifa hutoa fursa kufanya biashara ndogo ndogo kuleta bidhaa zao na kukatwa kodi inayoingia moja kwa moja kwenye manispaa hiyo. 
Alisema mapato mengine ya serikali hutokana na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), inayokatwa kwa kila mchezo ambayo hukusanywa na TRA. 
Hata hivyo, kiasi cha fedha ilichopata serikali ndani ya miaka saba kililalamikiwa na wabunge wengi kwamba ni kidogo. 
Katika swali lake la nyongeza, Mturano amedai kiwango hicho ni kidogo sana na kwamba, kuna harufu ya ufisadi katika makusanyo ya mechi za soka na shughuli nyingine zinazofanyika katika uwanja huo. Mbunge huyo alisema, kuna mianya mingi ya ufisadi katika fedha hizo. 
Akitolea mfano wa moja ya magazeti ya hivi karibuni, lililoripoti kwamba mamilioni ya makusanyo ya fedha hizo hupelekwa TFF kwenye mifuko ya rambo. Mbunge huyo alisema hali hiyo inaweka wazi mianya ya ufisadi na kutaka serikali itoe majibu. 
“Majibu ya Mheshimiwa Waziri si sahihi kabisa. Kwanza Manispaa ya Temeke haipati chochote kutokana na uwanja huo kuwapo wilayani Temeke. Pili, nataka kujua kwanini fedha hizo zipelekwe kwenye rambo TFF?” alihoji mbunge huyo. 
Mbunge huyo alimtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa fedha zinazokusanywa kwenye uwanja huo. 
Katika swali lake la msingi, Mturano alitaka kujua, kuwa Manispaa ya Temeke ambayo ni mwenyeji wa Uwanja wa Taifa inanufaikaje na mapato ya uwanja huo. 
Pia alihoji, tangu uwanja huo uanze kutumika serikali imepata kiasi gani na kati ya hizo Manispaa ya Temeke imepata kiasi gani?
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA