LIGI DARAJA LA PILI MKOA WA DAR KUANZA APRILI 9

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimetangaza kuanza kwa Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam, hatua ya sita bora.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, amesema hayo leo Aprili 5 kuwa ligi hiyo itaanza Aprili 9 mwaka huu hadi 31 katika viwanja vitatu  vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kinesi na Makurumla.
Alizitaja timu zitakazochuana katika hatua hiyo kuwania kucheza Ligi ya Kanda Taifa kuwa ni pamoja na Boom FC ya Ilala, Friends Rangers ya Magomeni, Abajalo FC ya Sinza, Red Coast ya Mburahati, Day Break ya Magomeni na Shariff Star ya Ilala.
“Kwa mujibu wa ratiba yetu, kila siku kutakuwa na mechi tatu, hivyo katika mechi za ufunguzi Aprili 9, Boom FC wao watachuana na Shariff Star, kwenye Uwanja wa Airwing, wakati Day Break watamenyana na Friends Rangers uwanja wa Makurumla huku Red Coast wao watacheza dhidi ya Abajalo,” alisema Mharizo.
Timu tatu katika ligi hiyo zitawakilisha mkoa katika Ligi ya Kanda Taifa hapo baadae.
Wakati huo huo, Mharizo amesema kabla ya kaunza kwa ligi hiyo, kutatolewa semina elekezi kwa viongzi wa timu shiriki, itakayofanyika Jumapili kwenye Ukumbi wa Shule ya BenjaminMkapa kuanzia saa nne asubuhi.
“Lengo la semina hii elekezi ni kutoa elimu kwa viongozi na wachezaji ili kuondoa mvutano wakati wa ligi hiyo, nia yetu ni nzuri na tunapenda kuona ligi ikichezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa,” alisema Mharizo.
Semina hiyo itawahusisha Katibu, Mwenyekiti, Kocha, Nahodha na Waamuzi 16 watakaochezesha ligi hiyo.