KOCHA WA YANGA AOMBA KAZI CRANES


KAMPALA, Uganda

KOCHA Tom Saintfiet aliyeipa Yanga ubingwa wa Kombe la Kagame Julai 28, mwaka jana kwa kuifunga Azam mabao 2-0, ameomba kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Uganda kuziba nafasi ya Bobby Williamson aliyetimuliwa baada ya kuinoa timu hiyo kwa miaka mitano.
Williamson raia wa Scotland ametimuliwa kazi kutokana na timu hiyo kutopata matokeo mazuri katika kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Dunia hapo mwakani nchini Brazil.
Saintfiet, aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Namibia kwa miaka miwili na nusu kabla ya kuzinoa pia Ethiopia na Yemen, anaamini anaweza kuipatia mafanikio timu hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki.
“Nimekuwa nikiifutilia soka ya Uganda kwa miaka kadhaa. Ni kati ya timu zinazocheza soka ya kuvutia katika ukanda huku wachezaji wake wakiwa na vipaji vya kutosha,” alisema na kuongeza:
“Nilipokuwa nainoa Ethiopia, niliwaona wakicheza mechi za Cecafa na nilipokuwa nainoa Yanga ya Tanzania, nilikuwa na wachezaji wa Uganda katika timu, ni wachezaji wazuri sana ambao walikuwa msaada kwa timu kutwaa ubingwa Kagame mwaka jana,” alisema Sainfiet.
Saintfiet (40), alisema kwa mazingira hayo, kitendo cha Uganda kutocheza michuano ya mikubwa kama Kombe la Mataifa Afrika, ni kukosa bahati tu.
“Lakini sasa ni muda wa kusonga mbele zaidi,” alisema na kuongeza: “Wanaweza, nataka kuwasaidia. Uganda ni pekee yenye pointi tatu kwenye kampeni za kucheza fainali za kombe la Dunia nyuma ya vinara, kama itasghinda mechi mbili za nyumbani dhidi ya Liberia na Angola hapo Juni, itakuwa kwenye nafasi nzuri,” alisema.
“Mwakilishi wangu amezungumza na rais wa Fufa-Shirikisho la soka Uganda (Mulindwa) ameonekana ni kiongoni mwenye kiu ya mafanikio ya soka kwa nchi yake, nasubiri kuitwa, naamini nikifanikiwa tutashirikiana kujenga timu imara zaidi kuelekea Kombe la Dunia na Fainali zijazo za Mataifa Afrika za Morocco,”
Saintfiet mwenye cheti cha daraja la juu katika ufundishaji kinachotambuliwa na Shirikiisho la soka Ulaya (Uefa),
alianza kufungisha mchezo huo miaka 17 iliyopita.
Amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la soka Nigeria kabla ya kutema kibarua hicho kutokana na
malipo yake kuzua mzozo.