HANS POPPE AREJESHA TENA NGUVU ZAKE SIMBA SC


MWENYEKITI wa Simba, Mhe, Ismail Aden Rage, amemshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe (pichani), kwa kukubali kurejea kushikilia nyadhifa zake zote.
Poppe alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake za uongozi ndani ya Simba Machi 7 mwaka huu, kutokana na hali ya migogoro iliyokuwapo wakati huo.
Hata hivyo, Rage alikataa kujiuzulu huko kwa Poppe na akasema atamshawishi abadili maamuzi kwa manufaa ya Simba.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaarifu wana Simba popote walipo kwamba Poppe amerejea na yuko tayari kuitumikia Simba kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,” alisema Rage.
Kwa upande wake, Poppe alisema amerejea Simba kutokana na utulivu ulioanza kujitokeza klabuni na kwamba nia yake ni kuhakikisha klabu inafanya usajili mzuri na wa kiwango kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.