FID Q, PROF J FUNIKA BOVU TAMASHA LA VODACOM@COCO BEACH


Na Mwandishi wetu.
MKALI wamuziki wa Hip Hop nchini, Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay, juzi alifanya makubwa katika tamasha la wazi lililoandaliwa na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania nakufanyika katika Ufukwe wa Coco Beach.
Mbali na Jay, wengine waliokuwapo na kufanya makubwa katika tamasha hilo lililohudhuriwa na watu wengi, alikuwapo Dar Stamina na Fid Q, ambapo wote kwa pamoja walifanikiwa kuwapatia burudani za aina yake.
Tamasha hilo lililofanyika maalum katika Sikukuu ya Pasaka, liliandaliwa maalum kwa ajili ya kusherehekea na wateja wao, pamoja na kuelimishwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni ya hiyo, ikiwapo Cheka Nao na promosheni ya Mahela, inayowawezesha wateja kujishindia pesa taslimu.
Akizungumza katika tamasha hilo, AfisaUdhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude, aliwashukuru Watanzania kwenda kwa wingi katika tamasha hilo la bure na kushiriki pamoja katika tukio hilo la kiburudani.
Alisema kuwa katika tamasha hilo, wateja wao walikuwa wakipewa elimu jinsi mtandao wao unavyofanyakazi, ikiwapo kujulishwa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo kwa kupitia tukio hilo lililofurika watu wengi.
"Sisi kama Vodacom tunashukuru kuwa pamoja na mashabiki wa muziki katika tukio hili la wazi lililoandaliwa mahususi kwa ajili yao, huku tukiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja kwa huduma mbalimbali zinazotolewa.
"Tunawaahidi kufanya kazi kwa moyo, pamoja na kuendeleza promosheni zenye mguso wa aina yake, ikiwapo hii ya Vodacom Mahela, ambapo wateja wetu wanapata fursa ya kujishindia fedha taslimu kutoka kwetu," alisema Kaude.
Aidha, msanii Profesa Jay alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani kuwapatia burudani mashabiki wake na kuungwa mkono, sambamba na kuwaimbisha kila wimbo aliotaka kuimba katika tamasha hilo lililokuwa na mvuto wa aina yake.
Baada ya kushuka kwa msanii huyo, alitoa fursa ya Stamina kupanda, huku dakika kumi baadaye, Fid Q naye alipanda na kufanya shoo pamoja na mkali huyo wa Hip Hop anayekubalika na watu wengi kutokana na nyimbo zake kali, ukiwapo wa 'Kabwela'.
Tamasha la wazi la Vodacom lililofanyika kwa siku mbili katika ufukwe huo wa Coco Beach, ambapo wateja wao wote walipata fursa ya kushuhudia burudani hiyo bila kutoa kiingilio cha aina yoyote.