DRFA YAANZA KUONESHA MAKUCHA YAKE KWA WAKIUKAJI WA SHERIA


CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimemfungia mchezaji Sued Lucas wa Boom FC kwa mwaka mmoja baada ya kupatiakana na hatia ya kusaini timu zaidi ya moja.
Mchezaji huyo licha ya kufungiwa, klabu yake ya Boom FC, imetozwa faini ya Sh 200,000.
Kamati ya Rufaa ya DRFA, iliyokutana Aprili 11 mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake Salehe Njaa, kupitia Kanuni ya 50 (a) imemfungia mchezaji huyo Sued Lucas kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuitoza klabu yake faini ya Sh 200, 000 kwa mechi zote alizocheza na matokeo ya mechi zote alizocheza mchezaji huyo yatabaki kama yalivyo.
Mchezaji huyo alisaini Boom FC kwa kutumia jina la Sued Lucas, wakati huo huo akasaini timu ya Kumbukumbu kwa jina la Issa Rashid Mwamlima.
Hivyo Kamati ya Rufaa imeirudishia Boom FC pointi zake tatu na mabao 2-0, waliyoupata katika mechi yao dhidi ya Kumbukumbu, iliyochezwa Aprili Mosi mwaka huu, uwanja wa Msasani.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kumbukumbu kumwekea pingamizi mchezaji huyo dhidi ya Boom.
DRFA inapenda kusisisitiza uadilifu kwa wachezaji na kuheshimu Kanuni na taratibu zilizowekwa, kwa maslahi na maendeleo ya mpira wa miguu.
Kutokana na hatua hiyo, Ligi Daraja la Pili, hatua ya sita bora iliyokuwa ianze Aprili 9, ilisitishwa na sasa itaanza kesho Aprili 15 kwa mechi tatu.
Boom FC watacheza dhidi ya Shariff Star uwanja wa Airwing, Abajalo dhidi ya Red Coast, uwanja wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere na Friends Rangers watachuana na Day Break, uwanja wa Kinesi.
Imetolewa na Ofisa Habari wa DRFA

Mohamed Mharizo