AZAM YABANWA NA SIMBA SC TAIFA 2-2, YANGA SASA YAPUMUA KILELENI

Haruna Chanongo (kushoto) wa Simba akitafuta mbinu za kuwatoka wachezaji mapacha wa Azam, Kipre Tchetche na Kipre Balou kulia jioni ya leo

Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Simba SC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Matokeo hayo, yanaiongezea Azam pointi moja na kuwa 47, ikibaki nafasi ya pili, nyuma ya Yanga yenye pointi 52, wakati SImba inabaki nafasi ya nne kwa pointi zake 36, nyuma Kagera Sugar yenye pointi 37 nafasi ya tatu.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Orden Mbaga, hadi mapumziko Simba SC ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Chipukizi Ramadhani Singano ‘Messi’ aliunganishia nyavuni mara zote mbili dakika ya 10 na 14 pasi muruwa za Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kushoto.
Kipre Tchetche aliifungia Azam kwa penalti dakika ya 29, baada ya Khamis Mcha ‘Vialli’ kuangushwa kwenye eneo la hatari na William Lucian ‘Gallas’.
Refa Orden Mbaga alimpandisha jukwaani kocha Muingereza wa Azam, Stewart Hall dakika ya 31 ya kwa kutoa maneno machafu, akilalaimikia uchezeshaji wa refa huyo.
Kipindi cha pili, Azam walirejea kwa nguvu kusaka bao la kusawazisha na wakafanikiwa kutimiza azma yao dakika ya 72 baada ya Humphrey Mieno kuunganisha shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’. 
Baada ya hapo, timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu na kosakosa kadhaa pande zote mbili. 
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Haroun Chanongo/Edward Christopher, Abdallah Seseme, William Lucian/Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Singano na Mrisho Ngassa/Fliex Sunzu.
Azam FC; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Luckson Kakolaki/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk, Salum Abubakar, John Bocco/Abdi Kassim, Humphrey Mieno/Jabir Aziz na Kipre Tchetche.