AZAM WAFUZU, SASA KUMENYANA NA WANAJESHI WENGINE KUTOKA MOROCCO, FAR RABAT

Humphrey Mieno licha ya kumlamba chenga kipa wa Barack, lakini alikosa bao la wazi

Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC imefanikiwa kuingia Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, licha ya jioni hii kulazimishwa sare ya bila kufungana na Barack Young Contollers II ya Liberia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sare hiyo ya leo katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Pili, inamaanisha Azam imefuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, baada ya awali wiki mbili zilizopita kushinda 2-1 mjini Monrovia.
Kwa matokeo hayo, Azam FC sasa itamenyana na timu ya jeshi la Morocco, FAR Rabat wiki mbili zijazo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Adelaide Ali aliyesaidiwa na Amaldine Soulamane na Ibrahim Mohamed wote kutoka Comoro, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.
Timu hizo zilishambuliana kwa zamu katika kipindi cha kwanza na kosakosa zilikuwa za pande zote mbili.  
Tofauti na wengi walivyodhani kwamba B.Y.C. ni timu dhaifu kwa kufungwa nyumbani na Azam, timu hiyo leo iliwatoa jasho wenyeji na kama wangetumia vyema nafasi zao walizotengeneza hadithi ingekuwa tofauti.
Azam pia hawakuwa na bahati katika mchezo wa leo, kwani walitengeneza nafasi nyingi nzuri na wakashindwa kuzitumia.
John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Kipre Herman Tchetche, Kipre Michael Balou na Humphrey Mieno wote walikosa mabao ya wazi wakiwa wamebaki na kipa tu wa B.Y.C. Winston Sayouah.
Kipa wa B.Y.C., Winston Sayouah aliwaongoza wachezaji wenzake baada ya mechi kwenda kuwapungia mikono ya asante mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiwashangilia kwenye mchezo huo.  
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, Joackins Atudo, David Mwantika, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Humphrey Mieno/Abdi Kassim na Brian Umony/Khamis Mcha ‘Vialli’.
Barack Y.C.; Winston Sayouah, Karleo Anderson, Joseph Broh/Prince Kennedy, Cammue Tummomie, Prince Jetoh, Junior Barshall, Benjamin Gbamy, Abraham Andrews, Randy Dukuly/Erastus Wee, Mark Paye na Ezekiel Doe.