AZAM FC, WAGOSI WA KAYA KUKWAANA SIKU YA MUUNGANO

Timu za Coastal Union ya Tanga na Azam zitapambana Aprili 26 mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27 mwaka huu, lakini imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa fursa Azam kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.
Mechi hiyo itachezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa (Pwani), Vicent Mlabu (Morogoro) wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Mohamed Mkono wa Tanga. Charles Komba wa Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya 24.
Baada ya mechi ya Tanga, Azam itarejea Dar es Salaam siku inayofuata tayari kwa safari ya kwenda Rabat itakayofanyika Aprili 28 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa wikiendi ya Mei 3, 4 au 5 mwaka huu.
Keshokutwa (Aprili 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Iwapo Azam itafanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho kutakuwa na marekebisho ya ratiba ya VPL. Hiyo ni kutokana na raundi inayofuata ya Kombe la Shrikisho kuchezwa wikiendi ya Mei 17, 18 na 19 mwaka huu ambapo bado haijajulikana Azam itaanzia wapi (nyumbani au ugenini) iwapo itavuka.
Mechi nyingine za VPL mwezi ni Aprili 25 (Ruvu Shooting vs Simba- Uwanja wa Taifa), na Aprili 28 (Simba vs Polisi Morogoro- Uwanja wa Taifa).