JANA na leo,
zimetolewa habari tofauti kuhusiana na klabu ya Simba ambazo uongozi umeona ni
vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo
ufafanuzi wa taarifa hizo.
1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal
Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa
Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na
anataka alipwe zote jana.
Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda
mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba
walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa
kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi
wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya
mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua
hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno.
Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki
huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire
walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina
utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya
wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote
inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati
wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake
wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha
hizo.
Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa
kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na
fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba
itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba
kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za
udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC
imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili
kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya
England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike.
Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka
kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster
United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa
Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo
wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri
utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja
inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza kwamba ni
taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia watu na taasisi
mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Simba ni CREDIT WORTHY INSTITUTION !
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha
kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya jana.
Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria
kinaangukia katika kundi la FORCED IMPRISONMENT
kwa wamiliki kuwazuia watu kinguvu hotelini kwao. WAMILIKI hawakutoa
notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya kuchukua
hatua hiyo.
Lengo lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa
hoteli ambayo imetoka kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi
wa Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu
zote, akili zetu zote na maarifa yetu yote.
2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA
KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba
wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina ukweli
wowote.
Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi
la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi husika. Uongozi
hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa benchi la ufundi.
Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa. Pia
uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga,
kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli kwani daktari huyo ana
ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana.
HITIMISHO
KATIKA namna ya kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda
kutoa shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa Taifa
na kuisapoti timu kwa asilimia 100. Uongozi unathamini sana mchango wa
wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza kuwarejeshea tena furaha
mioyoni mwao.
Uongozi pia unatumia nafasi hii kuwapongeza wachezaji na
benchi la ufundi ambao walicheza mechi ya jana katika mazingira magumu.
Walicheza bila ya kufanya warm up na wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini jambo
ambalo lingeweza kuwaondoa mchezoni.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
Comments
Post a Comment