YANGA YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA NEMBO ZAKE, WATAKAOKIUKA KUKUMBWA NA MKONO WA SHERIA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Klabu ya YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB (YANGA) ambayo ndiyo Klabu kongwe kabisa ya mpira hapa Tanzania, inatoa taarifa hii rasmi, kuzuia matumizi ya nembo ya Klabu kama inavyoonekana hapo juu.
TAARIFA hii inatolewa kama tahadhari na angalizo kuwa NEMBO ya YANGA ni nembo iliyosajiliwa rasmi kwa Msajili wa TRADEMARKS na inamilikiwa na KLABU ya YANGA. Trade Mark hiyo ilisajiliwa iliyosajiliwa tarehe June 02, 2009.
Kwa miaka mingi, kumekuwepo na tabia kwa wafanya biashara mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi kujihusisha na utengenezaji, uingizaji na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya YANGA.
YANGA inapenda kutoa angalizo kuwa tabia hiyo iliyokithiri ni ukiukwaji wa Sheria na unaikosesha Klabu mapato halali ambayo ingeyapata kutokana na matumizi ya Nembo yake.
Kwa mantiki hiyo, kuanzia leo hii, YANGA inatangaza rasmi kuwa ni marufuku kwa  kampuni, mtu binafsi au kikundi chochote kutengeneza ama kuuza bidhaa zenye nembo ya YANGA bila ridhaa ya Klabu ya YANGA. Iwapo itatokea mtu yoyote kukiuka taarifa hii, basi YANGA itachukua hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hii mbaya ya KINYONYAJI.
Klabu ya Yanga imepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyabishara na watu mbalimbali ambao wanajihusisha na utengenezaji wa bidhaa zenye nembo ya YANGA ambao wanakusudia kuingiza bidhaa mbalimbali nchini zenye nembo ya YANGA kwa nia ya kuziuza.  
YANGA inatoa tahadhari kuwa kitendo hicho ni uvunjaji wa sheria na matumizi yasiyo halali ya nembo yake na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
YANGA inawashauri wale wote wanaotaka kuingiza bidhaa au kuuza bidhaa zenye nembo yake wawasiliane na uongozi wa Klabu ili waweze kuingia makubaliano rasmi kwa yule ambaye atakubaliwa kuingiza bidhaa hizo zikiwa ni zenye kiwango na ubora ambao utakubaliwa na kupitishwa na YANGA.
Mtu yeyote mwenye nia hiyo basi awasiliane na KATIBU MKUU wa Klabu Ndugu LAWRENCE MWALUSAKO katika Makao Makuu ya Klabu Mtaa wa TWIGA/JANGWANI, Dar es Salaam.
MWISHO kabisa, YANGA inatoa wito kwa wanachama na wapenzi wake kutonunua bidhaa zozote zenye nembo ya YANGA Iwapo muuzaji huyo hajaruhusiwa rasmi na YANGA kwani tabia hiyo inaikosesha KLABU mapato na kuifanya kuendelea kuwa tegemezi.

Imetolewa Dar es Salaam tarehe 22 March 2013.
LAWRENCE MWALUSAKO