YANGA WAENDELEA KUPIGA JARAMBA


Kikosi cha Young Africans kilipokuwa katika kambi ya mafunzo nchini Uturuki


Kikosi cha timu ya Young Africans leo kimeendelea na mazoezi katika katika uwanja wa mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo namba 135 wa mzunguko wa pili wa Ligi ya Vodacom dhidi ya timu ya Toto African siku ya jumamosi  Machi 09 ,2013 katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
 
Mara baada ya kupata ushindi wa tatu mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, kikosi cha mholanzi Ernest Brandts kiliendelea na mazoezi katika Uwanja wa mabatini Kijitonyama tangu siku ya jana ikiwa ni maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Toto African.
 
Young Africans ambayo inapongoza msimamo wa VPL kwa kuwa na pointi 42 na mabao 35 ya kufunga, inahitaji kushinda kila mchezo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Kuu ya Vodacom ambayo kwa sasa imefikia katika ya mzunguko wa 18.
 
Katika mchezo wa mwisho Young Africans iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Kagera Sugar bao lililofungwa na kiungo Haruna Niyonzima, tangu mzunguko wa pili uanze Yanga imeshacheza jumla ya michezo mitano na kufanikiwa kushinda michezo minne na kutoka sare mmoja hivyo kujikusanyia point 13 kati ya 15.
 
Kocha Mkuu Ernest Brandts mara baada ya mazoezi ya leo, amewapa mapumziko wachezaji wake ya siku mbili (jumamosi na jumapili) ili waweze kupata nafasi ya kujumuika na familia zao mwishoni mwa wiki, na mazoezi yataendelea tena siku ya jumatatu asubuhi katika uwanja wa mabatini Kijitonyama.