YANGA, V RUVU SHOOTING HAPATOSHI uWANJA WA TAIFA LEO


VINARA wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) Yanga Sc leo watashuka katika uwanja wa Taifa kuwakabili maafande wa Ruvu Shooting katika muendelezo wa hatua za lala salama ya ligi hiyo.

Yanga ambayo tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo haijapoteza hata mchezo mmoja, itashuka dimbani kwa lengo moja tu la kushinda ili kujipatia pointi tatu zitakazowaweka katika mazingira mazuri ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwani tayari Shooting imeshatoa hadhari kwa vinaraha hao kwa kuhakikisha inavunja mwiko wa kutofungwa tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo, kabla ya kuondoka na pointi tatu muhimu.

Akizungumzia mchezo wa leo Ofisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema kwamba kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo na kwamba watashusha silaha za maangamizi, lengo ikiwa ni kuhahakikisha wanashinda mchezo huo.

Alisema anafahamu Shooting wamejipanga vizuri kwa lengo la kushinda mchezo huo lakini ni kama ndoto na kamwe wasitarajio ndoto hizo kuwa kweli.

“TUnasikia tu Shooting wanavyochonga kwenye vyombo vya habari lakini hilo halitupi hofu kwani sisi tumejiandaa kukabiliana na timu yoyote tutakayokutana nayo, hivyo maafande nao wasubiri kipigo kama timu nyingine tulizokutana nazo awali,”aliongeza

Kizunguto aliongeza kuwa wachezaji wa timu hiyo ukiacha   Ladislaus Mbogo ambaye ni anauguza jeraha baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe  kwenye shavu, pia Kelvin Yondani  anayesumbuliwa na uvimbe kwenye kidole gumba cha mguuni na Stephano Mwasika anaye majeruhi ambao wataukosa mchezo wa leo, nyota wengine wote wapo katika hali nzuri.

Yanga yenye pointi 45, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili ligi hiyo, imeshacheza jumla ya michezo sita ambapo imeshinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja, katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo iliitandika Shooting mabao 3-2.

Naye Ofisa habari wa  Ruvu Shooting  Masau Bwire alisema timu yake ipo tayari kwa mchezo wa leo na kwamba wamedhamiria kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira ya kuwania ubingwa.

Alisema Ruvu Shooting haiidharau Yanga lakini uwezo wa kusakata kabumbu walionao wachezaji wake unawapa kujiamini na uhakika wa kushinda mchezo huo ambao anaamini utakuwa na ushindani mkubwa kwani Yanga hawatakubali kirahisi kuupoteza.

Aliongeza kuwa timu yake itaudhihirishia umma wa Watanzania hususani wapenza soka kwamba soka la Tanzania si la Yanga na Simba, bali zipo timu zenye uwezo wa kucheza zaidi yao hususani Ruvu Shooting ambapo amejigamba timu yake kuibuka na mabao ya kutosha.

Bwire aliwataka waamuzi wa mchezo huo kuchezesha kwa kufuata sheria 17 za soka ili mshindi apatikane kwa uwezo wa uwanjani na si kubebwa, huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani na hasa mashabiki wa Simba watakaofarijika na matokeo hayo kuja  kushuhudia maarifa ya sisimizi kumuua tembo.

Mchezo huo ambao utachezeshwa na mwamuzi Jacob Adong wa Mara, viingilio vitakuwa sh 5,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh 8,000 kwa viti vya orange, sh 15,000 kwa watakaokaa VIP B na C huku watakaokaa VIP A watalipa sh 20,000.
Mbali na mechi hiyo ya Yanga na Ruvu Shooting, mchezo mwingine wa ligi hiyo leo utakuwa kati ya Toto Africans ya Mwanza itakayoikabiliMgambo Shooting katika uwanja wa CCm Kirumba Mwanza, huku Mtibwa Sugar itakipiga na Coastal Union ya Tanga katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro.