YANGA HAKUNA KULALA MPAKA KIELEWEKE


Kikosi cha timu ya Young Africans leo kimeendelea na mazoezi asubuhi katika uwanja wa mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi ya Vodacom dhidi ya timu ya Toto African siku ya jumamosi  Machi 09 ,2013 katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuwa na pointi 42 na mabao 35 ya kufunga na mabao 12 ya kufunga, iko mbele kwa pointi sita zaidi ya timu ya Azam inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na ponti 36 na mabao 31 ya kufunga na mabao 15 ya kufungwa.
Mara baada ya kupata ushindi wa tatu mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, kikosi cha mholanzi Ernest Brandts kiliendelea na mazoezi katika Uwanja wa mabatini Kijitonyama siku ya alhamis na ijumaa kabla ya kupewa mapumziko ya siku mbili jumamosi na jumapili.
Katika mchezo wa mwisho Young Africans iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Kagera Sugar bao lililofungwa na kiungo Haruna Niyonzima, tangu mzunguko wa pili uanze Yanga imeshacheza jumla ya michezo mitano na kufanikiwa kushinda michezo minne na kutoka sare mmoja hivyo kujikusanyia point 13 kati ya 15.
Ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa Ubingwa, Kocha Mkuu Brandts amesema anakianadaa kikosi chake kuhakikisha kinapata pointi 3 katika kila mchezo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa Ubingwa.
Kila mchezo tunaocheza kwa sasa ni fainali kwetu, kila timu inahitaji kupata pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri, na sisi pia tunahitaji  kupata pointi 3 katika kila mchezo hali inayopelekea mechi kuwa ngumu, lakini kikubwa nimekiandaa kikosi changu kuhakikisha kinaibuka na pointi 3 katika kila mchezo alisema 'Brandts'.
HABARI:www.youngafricans.co.tz