YANGA HAIKAMATIKI


TIMU ya Yanga imezidi kuyoyoma kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara, baada ya leo kushinda bao 1-0 dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting ya Pwani katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga sio tu imeendeleza rekodi yake ya kutofungwa tangu kuanza raundi ya pili ya ligi hiyo, Januari 26, pia imezidi kuukaribia ubingwa wa ligi hiyo iliyoanza Septemba 15, mwaka huu.
Yanga sasa inaongoza ligi hiyo yenye timu 14 kwa pointi 48 ilizovuna katika mechi 20 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 37 na mabingwa watetezi Simba wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi 34, wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya Yanga.
Katika mechi ya leo,bao pekee lililopeleka pointi tatu Jangwani, lilifungwa dakika ya 48 na nyota wake wa kimataifa wa Uganda, Hamis Kiiza  akimalizia krosi maridadi ya Nizar Khalfan.