WEMA AMWOKOA KAJALA KWENDA JELA, AMLIPIA FAINI YA MILIONI 13

NA FURAHA OMARY
MSANII nyota wa filamu nchini Wema Sepetu, amemnusuru msanii mwenzake wa fani hiyo, Kajala Masanja kwenda kutumikia kifungo cha miaka 12 jela, baada ya kumlipia faini ya fedha taslim sh. milioni 13.
Wakati Kajala, ambaye amesota rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja akinusurika na kifungo hicho kutokana na adhabu iliyotolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mumewe Faraja Chambo, alihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12 kutokana na kushindwa kulipa faini ya sh.milioni 213.
Kajala na mumewe Chambo, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Marchi 15, mwaka jana, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama ya kubadilisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala, Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Akisoma hukumu hiyo jana katika ukumbi namba moja wa mahakama uliokuwa umejaa wasanii wa filamu, akiwemo Elizabeth Michael au Lulu, Mansour Awadh ‘Dk. Cheni’ na Wema, Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, alisema katika shitaka la kula njama, mahakama imejiuliza iwapo ni kweli washitakiwa, ambao ni mke na mume walikaa na kupanga kuuza nyumba hiyo.
“Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi na hoja za kisheria zilizowasilishwa, mahakama inajiuliza kama kweli washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa. Hakukuwa na pingamizi kutoka kwa mawakili wa pande zote kwamba washitakiwa walikaa na kuuza nyumba na uuzaji huo ulikuwa halali au la,” alisema Hakimu Sundi alipokuwa akisoma hukumu hiyo huku Kajala, ambaye alikuwa katika kizimba akiangua kilio.
Hakimu Sundi alisema katika shitaka la pili, mahakama imeridhika na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka kwamba kulikuwa na notisi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuzuia uuzaji wa nyumba.
Alisema kutokana na ushahidi huo, mahakama imewatia hatiani washitakiwa wote kwa sababu si kweli walikuwa hawafahamu kulikuwa na notisi hiyo, lakini waliidharau na kuuza nyumba.
Kuhusu shitaka la tatu la kutakatisha fedha haramu, Hakimu Sundi alisema mahakama inamtia hatiani mshitakiwa Chambo, kwa sababu imeridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka, kwamba wakati anafanyakazi katika benki ya NBC, alipata fedha kwa michezo aliyokuwa anaijua na kujenga nyumba na baadae kuficha ukweli kwa kuiuza baada ya TAKUKURU kujua hilo.
Hakimu Sundi alisema kuwa, Kajala hana hatia katika kosa hilo kwa kuwa hahusiki katika upatikanaji wa fedha hizo zilizotumika kujengea nyumba.
“Mahakama inawatia hatiani washitakiwa wote kwa kosa la kwanza na la pili na kosa la tatu linamtia hatiani Chambo pekee,” alisema Hakimu Sundi.
Baada ya kutiwa hatiani washitakiwa hao, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, alidai hana kumbukumbu za makosa kwa mshitakiwa Kajala, lakini Chambo ana shitakiwa mahakamani hapo kwa makosa mengine.

Swai aliiomba mahakama hiyo, kutoa adhabu kali dhidi ya washitakiwa kwa kuwa makosa ya utakatishaji fedha haramu yamekuwa tatizo katika nchi na kwamba washitakiwa hao walikaidi amri ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kutouza kwa nyumba hiyo.
“Naomba washitakiwa wapewe adhabu kali kwa mujibu wa sheria husika ya utakatishaji fedha haramu,” aliomba Swai.
Kwa upande wa wakili wa washitakiwa, Barnarbas Lubuwa, aliiomba mahakama wakati inafikiria adhabu, ikumbuke kwamba washitakiwa, ambao ni mume na mke wana familia inawategemea, ambapo inaweza kuwaumiza wazazi huku familia ikiathirika.
Pia, alidai Kajala hajui upatikanaji wa fedha hizo, ambapo kuhusika kwake ni kutia saini mbele ya wakili kwa nafasi yake ya mke katika suala la uuzaji wa nyumba. Aliiomba mahakama katika kutoa adhabu izingatie mazingira.

HAKIMU ATOA ADHABU

Hakimu Sundi alisema katika shitaka la kula njama, washitakiwa walipe faini ya sh. milioni tano au kifungo cha miaka miwili jela. Shitaka la pili, washitakiwa walipe faini ya sh. milioni nane au kifungo cha miaka mitano na shitaka la tatu, ambalo ametiwa hatiani Chambo peke yake, alipe faini ya sh. milioni 200 au kifungo cha miaka mitano jela.

HALI ILIVYOKUWA BAADA YA ADHABU
Baada ya Hakimu Sundi kutoa adhabu hiyo, Kajala ambaye wakati hukumu hiyo ikitolewa, alikuwa akiangua kilio, aliendelea kulia kwa uchungu jambo lililowaliza wasanii wenzake na ndugu na jamaa zake waliokuwepo mahakamani hapo.
Mbali ya Kajala, mama mkwe wake naye alishindwa kujizuia, ambapo kwa wakati wote alikuwa akilia hadi washitakiwa hao walipopelekwa mahabusu wakisubiri hatma yao.
Akiwa katika chumba cha mahabusu, Kajala alikuwa akilia kwa wakati wote hali iliyowafanya washitakiwa wenzake kumfariji kwa kumbembeleza.
Kajala alipokuwa mahabusu, wasanii Cheni na Wema walikuwa wakihangaika huku na huko kuhakikisha wanamnusuru kwenda jela, ambapo waliamua kuitisha kikao cha wasanii wote na baadae Wema kuamua kwenda benki kuchukua fedha.

WASANII WAHAHA KUMNUSURU
Dk. Cheni alisema kuwa, Mwenyezi Mungu amesikia maombi yao kwa Kajala kutokana na mahakama kutoa adhabu ya kulipa faini au kifungo.
“Mwenyezi Mungu amesikia maombi yetu kwa Kajala. Tunashukuru kwa hilo. Tumekutana na kuchangishana, hata hivyo Wema amesema atalipa yeye faini yote na sasa ameenda benki kuchukua fedha,” alisema Dk. Cheni.
Baada ya Wema kurejea na kitita hicho cha fedha, nyuso za furaha zilitawala kwa Kajala, ndugu na jamaa zake ambapo baada ya kulipa faini hiyo, vicheko vilitawala mahakamani hapo, hali iliyowalazimu askari kuwaondoa wasanii hao na kwenda eneo la kusubiria kesi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Wema alisema kuwa ametoa fedha hizo kwa moyo mmoja kwa kuwa Kajala ni zaidi ya rafiki na zaidi ya ndugu.
“Kajala rafiki yangu, ndugu yangu na ni zaidi ya ndugu, kumsaidia kwangu sijaona kama nimepoteza, najua Mwenyezi Mungu atanilipia,”alisema Wema

KAJALA HUYOOOOOOO
Baada ya kutoka mahabusu, Kajala alimkumbatia mama yake mzazi, mdogo wake na wasanii wenzake, akiwemo Lulu huku akilia, jambo lililoangua vilio kwa wengine waliokuwa wakimsubiri wakiwemo ndugu zake.
Hata hivyo, msanii huyo hakuruhusiwa kuzungumza na mtu yeyote baada ya ndugu zake kumtaka aingie katika gari lililokuwa likimsubiri ili aende akapumzike nyumbani.

Habari/Picha na Liwazo zito blog