Wachezaji wa Ligi Kuu
ya Soka Tanzania Bara na Zanzibar wenye umri kati ya miaka 18 na 21 wametakiwa
kuchangamkia fursa ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Barani
Ulaya, Asia na Afrika wakiwa nyumbani Tanzania.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, Teonas Aswile,
waandaaji wa Michuano ya African Youth Football Tournament amesema kuwa katika michuano
hiyo wachezaji 11 bora watatafutiwa timu moja kwa moja katika mataifa nane
barani Ulaya (Ufaransa, Ureno, Uholanzi, Denmark, Norway, Sweden, Ubelgiji na
Switzerland), Asia na Afrika.
Bwana Teonas Aswile
amesema kuwa wachezaji wa Tanzania bado hawajaonesha muamko mkubwa licha ya
kiwango cha chini cha kushiriki ambacho wamewekewa ikilinganishwa na wachezaji
wa kigeni, ambao licha ya kuwekewa USD 500 bado wamezidi kumiminika.
“Mpaka sasa kuna
mawakala wawili ambao tumezungumza nao na wamethibitisha kuleta wachezaji wao
zaidi ya 20 kushiriki kwenye michuano.”
“Hii ni mbali ya
wachezaji mmoja mmoja ambao tunaowasiliana nao ambao wanataka kuja, wakiwa
zaidi ya watano. Kwahiyo wachezaji wetu waamke na kuitumia fursa hii ambayo
haipo katika nchi nyingine ya Afrika kwa wachezaji kufanya majaribio nchini
mwao.”
Aidha Aswile
ameviomba vilabu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwalipia wachezaji wake ada ya
shilingi laki tatu (Tsh 300, 000) ambayo inahitajika kwa mchezaji ili aweze
kushiriki kwenye michuano ya African Youth Football Tournament kufanya hivyo
kwani mchezaji huyo atakapouzwa klabu husika ndiyo itakayokubaliana na klabu
itakayomchukua na si Kampuni ya Tanzania Mwandi.
“Sisi tunachokifanya
ni kumuwezesha mchezaji aone njia za kufikia malengo yake. Kwa hiyo
akishafanikiwa na amepata timu ya kuchezea iwe Ulaya, Asia au Afrika, klabu
yake ndio itakayokubaliana na timu ya huko sisi hatutachukua chochote”, Teonas
alisema.
Mkurugenzi huyo
akitaja idadi ya wachezaji wa Tanzania ambao tayari wamethibitisha kushiriki
amesema kuwa ni wachezaji watatu jambo ambalo bado linaonyesha mwamko umekuwa
mdogo.
Michuano ya African
Youth Football Tournament itafanyika Tanzania katika uwanja wa Karume jijini
Dar es Salaam kuanzia tarehe 10 hadi 14 mwezi wa sita mwaka huu na
kuwashirikisha wachezaji wenye umri wa miaka 18 hadi 21 ambapo watafundishwa na
makocha watatu kutoka nje ya nchi na wawili wa Tanzania.
Pia michuano hiyo
itashirikisha mawakala kutoka nchi nane za barani Ulaya, Asia na Afrika ambao
wanahitaji wachezaji kwaajili ya klabu wanazoziwakilisha kati yao wakiwa ni Budak
Johan, Cabrera Oliver, Dag Larsson, Phillip Mwakikosa na Dahlin Martin huku
wakala wa kimataifa wa Tanzania Dr Damas Ndumbaro akiwa miongoni mwa mawakala
wa Tanzania watakaoshiriki katika michuano kusaka vipaji kwaajili ya klabu
mbalimbali.
“Tuna maombi ya
mawakala wawili ambao wanataka wachezaji mabeki, washambuliaji na viungo
kwaajili ya klabu zao Kuwait, Qatar, Libya na sehemu nyingine kwa hiyo hii ndio
fursa ya wachezaji wetu kwenda kucheza soka la kulipwa na lenye maslahi zaidi
kwao.”
Comments
Post a Comment