TFF:MKUTANO WA DHARULA SIMBA SI HALALI

Aden Rage, Mwenyekiti wa Simba Sc

Mkutano Mkuu wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17
mwaka huu na kuuondoa uongozi wa klabu hiyo si halali kwa vile
haukufuata taratibu, na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
halitambui Kamati za Muda.

Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
jana (Machi 24 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti
wake Alex Mgongolwa.

Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba,
Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa na Kamati ya Utendaji baada ya
wanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi na
kujiorodhesha. Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji ya
Simba.

Utaratibu huo haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa
Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya
Simba ambayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Simba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha
Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama
waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.

Kamati imesisitiza kuwa Katiba za wanachama wote wa TFF hazina
kipengele cha kura ya kutokuwa na imani na uongozi (vote of no
confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga, Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.

Hata Katiba ya Simba haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura
kufukuza uongozi uliochaguliwa.

Katiba za wanachama wote wa TFF zimezingatia katiba mfano za
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambazo zinasema
kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si kuteuliwa (Kamati ya
Muda).

Pia Kamati imesema endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na
uongozi ukakataa kuitisha mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF
kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa mwongozo kwa uongozi wa Simba .

TFF ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa viongozi wa wanachama wake
wanaokwenda kinyume cha Katiba zao. Pia Kamati imesisitiza kwa
wanachama wa TFF kuitisha mikutano yao kwa mujibu wa taratibu na
Katiba zao, na wale ambao muda umefika wafanye hivyo haraka.