TFF YAUNGA MKONO KAULI RAIS JAKAYA KIKWETE KUHUSIANA NA VILABU VYA TANZANIA


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeunga mkono kauli iliyotolewa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ya kuzitaka timu za ligi kuu kuiga mfano wa Azam kwa kuhakikisha zinaanzisha timu za vijana na kuwa na viwanja vyao.
Rais Kikwete aliyasem hayo wakati akizindua uwanja wa kisasa unaomilikiwa na timu ya soka ya Azam Fc ulipo Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.
 Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kwamba, kwa muda mrefu TFF imekuwa ikivihimiza vilabu hivyo kufanya hivyo lkini vimekuwa haviutuilii mkazo suala hilo.
Alisema wanashukuru Rais kikwete ameliona hilo na kulikumbushia kwa mara nyingine hivyo TFF inaamini viongozi wa vilabu husika watalipa kipaumbe suala hilo.
“Tunapongeza kauli ya Kikwete kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukisisitiza timu kuwa na timu za Vijana pamoja na viwanja vyao lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo,”alisema Osiah.
Kati ya timu 14  zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom ni Azam na Mtibwa Sugar pekee zenye viwanja hai ambavyo vinaweza kutumika kwa michezo ya ligi hiyo, huku timu kama Yanga ina walau uwanja wa kufanyia mazoezi.
Aidha, kwa upande wa timu za vijana timu zote zinazoshiriki ligi hiyo zinamiliki timu za vijana isipokuwa ni timu chache ikiwemo Azam, Mtibwa Sugar, Yanga na Simba ndizo zinazotilia mkazo kuwekeza kwa timu za vijana.