TFF YAONDOA ‘FREE PASS’ MPIRANI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeondoa utaratibu wa wadau wake kuingia bure kwenye mechi kwa kutumia tiketi maalum (free pass).

Kutokana na uamuzi huo hakutakuwa tena na pasi za bure kwa ajili ya kushuhudia mechi zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa TFF katika viwanja mbalimbali nchini.

Uamuzi huo umetokana na ukweli kuwa free pass zimekuwa zikipunguza au kuchukua mgawo wote wa TFF kwenye mechi, na wakati mwingine Shirikisho hulazimika kutoa fedha za ziada kugharamia pasi hizo.

Pasi zote ambazo imekuwa ikitoa kwa wadau wake hukatwa katika mgawo wa TFF katika mechi husika. Shirikisho hivi sasa linapata asilimia nne tu ya mapato katika mechi za Ligi Kuu, ligi ambayo hivi sasa inaendeshwa na Kamati yake ya Ligi.