Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amewataka viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa
kuhakikisha wanaingiza wachezaji wenye umri sahihi katika michuano ya U15 FIFA
Copa Coca-Cola 2013.
Ametoa mwito huo leo (Machi 26 mwaka huu) wakati akifungua
semina elekezi ya michuano ya Copa Coca-Cola ambayo kuanzia mwaka huu itakuwa
ikishirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 15.
Rais Tenga amesema hakuna jambo la kipuuzi kama
kuchomekea wachezaji ambao wamezidi umri unaotakiwa kwa vile lengo la michuano
ya aina hiyo ni kubaini vipaji na kuwafanya watoto wapende kucheza mpira wa
miguu.
“Kwanza nawashukuru kwa
kutenga muda wenu na kuhudhuria semina. Lakini ni vizuri pia mkahakikisha
mnakuwepo kwenye mashindano ili kutekeleza haya ambayo tutakubaliana katika
semina hii. Mkileta mtu mwingine anaweza kutuanzishia mambo mengine badala ya
yale tutakayokubaliana,” amesema Tenga.
Pia ameishukuru kampuni ya Coca-Cola ambaye imekuwa
ikidhamini michuano hiyo tangu mwaka 2007 ambapo semina hiyo elekezi
inayoshirikisha makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na waratibu wa
mikoa wa michezo ya UMISSETA ni ya saba mfululizo.
Ratiba ya michuano hiyo kuanzia mwaka huu imebadilika ambapo
sasa itaanzia ngazi ya wilaya Aprili wakati fainali katika ngazi ya Taifa
itachezwa Septemba.
Comments
Post a Comment