SIMBA YAWASILI ANGOLA, BOBAN NA BASENA WABAKI DAR KWA MATATIZO TOFAUTI

Boban

Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
SIMBA imetua nchini Angola leo asubuhi na tayari wenyeji wao –Libolo, wameipeleka katika mji wa Calulo uliopo katika jimbo la Kwanza Sul.
Mji wa Calulo (inatamkwa kalulu) upo umbali wa takribani dakika 35 kwa ndege kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda ambako Simba ilifika majira ya saa nne asubuhi.
Simba imekuja Angola kwa ajili ya kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Libolo ambayo ilishinda katika mechi ya kwanza kwa bao 1-0.
Wekundu wa Msimbazi wamewasili Angola bila ya kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi ‘Boban’ na meneja wa timu, Moses Basena.
Boban alishindwa kusafiri na timu baada ya kushikwa na malaria kali saa chache kabla ya safari na baada ya vipimo ikaonekana kwamba haitakuwa vema kwake kusafiri.
Basena naye hakujiunga na msafara kwa vile alipata taarifa za kulazwa hospitali kwa mkewe nchini Uganda na uongozi wa Simba ukampa ruhusa ya kwenda kumuuguza.
Hata hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba ambaye ndiye kiongozi mkuu wa klabu katika timu nchini Angola, Zacharia Hans Poppe, alisema anaamini wachezaji waliobaki bado wanaweza kufanya kazi nzuri.
“Tungependa kuwa na Basena na Boban hapa lakini Mungu ndiye mpangaji wa yote. Hatuwezi kushindana naye. Cha msingi ni kwa wale waliopo kufanya kazi ambayo Wana Simba wanaitarajia,” alisema.
Poppe ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, alisema kwa bahati nzuri kikosi cha Simba kina wachezaji wengi wa kitaifa na kimataifa na ndiyo hana wasiwasi na mechi hiyo hiyo ya marudiano.
Simba imepokewa vema nchini Angola ambapo viongozi wa Libolo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Augusto Correia, pamoja na viongozi wengine waliulaki msafara wa Wekundu wa Msimbazi katika Uwanja wa Ndege wa Februari 4, jijini Luanda.
Libolo pia walitoa usafiri wa ndege kwa msafara wa Simba kutoka Luanda hadi Calulo kwa vile mji huo uko umbali wa zaidi ya kilomita 200 kutoka mji mkuu na kwa mujibu wa ibara ya tano kifungu cha nne cha kanuni za CAF, usafiri wa basi usingekubalika.
Jana jioni Simba ilitarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja ambao imepangiwa na wenyeji wao lakini kesho ni lazima ifanyie mazoezi katika Uwanja wa Estadio Municipal De Calulo ambako mechi hiyo itachezwa.
Wawakilishi wa Libolo waliokuja kuipokea Simba walionyesha kuvutiwa zaidi na uwezo wa mchezaji Mrisho Ngassa na Correia aliwasilisha rasmi nia ya kutaka kumsajili nyota huyo wa Taifa Stars.
Katika mazungumzo yake na Poppe, Correia alisema wanataka kuzungumza na uongozi wa Simba lakini Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Usajili akasema inabidi Libolo wasubiri kwanza mechi ichezwe.
Mji wa Calulo ni mdogo sawa na miji mingine midogo ya Tanzania na kuna ukosefu wa baadhi ya huduma muhimu za kijamii.