SIMBA WAZUNGUMZIA KIPIGO CHA LIBOLO, KUREJEA KESHO USIKU


Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
TIMU ya Smba inarejea nchini Tanzania kesho usiku ikitokea Angola ambako jana ilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Libolo ya hapa.
Wachezaji wa Simba leo asubuhi wamefanya mazoezi katika Uwanja wa Libolo uliopo hapa ambako mechi hiyo ilichezwa na mchana itasafiri kwenda mji mkuu wa Angola, Luanda, itakapolala kusubiri safari ya kesho.
Hali katika kambi ya Simba iliyopo katika Hoteli ya Ritz, ilikuwa ya huzuni kutokana na kipigo hicho kikubwa zaidi cha ugenini ambacho Simba imewahi kukipata katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mara ya mwisho Simba kupata kipigo kikubwa ilikuwa mwaka 2009 ilipofungwa mabao 5-1 na Harass Al Hadoud ya Misri katika michuano kama hii kwenye mechi iliyopigwa jijini Alexandria, Misri.
Kwa ujumla, Simba ilicheza vizuri katika mchezo huo isipokuwa katika dakika 10 za mwisho ambazo iliruhusu mabao matatu kati ya manne iliyofungwa.
Hata hivyo, matokeo hayo ya 4-0 hayatoi tathmini halisi ya mechi hiyo kwa vile katika sehemu kubwa ya mchezo huo, Simba na Libolo zilikuwa zimetoshana nguvu.
Libolo walikuwa na faida ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa kama vile kiungo Ruben aliyekuwa nyota wa mchezo huo ambaye pamoja na kufunga bao la tatu, ndiye aliyekuwa akiichezesha timu hiyo.
Ruben ametoka kuichezea klabu ya Braga ya Ureno iliyokuwa ikishiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na tofauti za wachezaji kama hao na wale wa Simba ilionekana katika namna ambavyo wenyeji walitumia nafasi zao.
Saa moja kabla ya mechi kuanza, mvua kubwa ilinyesha katika mji wa Calulo na kuathiri hali ya uwanja jambo lililosabisha mpira kuchezwa katika mazingira magumu.

Comments