KUMEKUWAPO na taarifa za kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa
Wanachama wa Simba uliopangwa kufanyika Kesho (Machi 17, 2013) jijini Dar es Salaam kujadili
mustakabali wa klabu.
Ikumbukwe kwamba Mkutano Mkuu wa Wanachama ndiyo chombo cha
juu kabisa cha maamuzi kwa klabu yetu. Katiba ya Simba SC
imeupa Mkutano Mkuu hadhi ya juu mno na ndiyo maana imeweka utaratibu wa
kufanyika kwake.
Miongoni mwa utaratibu ni kwamba ni lazima uitishwe na
Mwenyekiti aliye madarakani wa klabu. Kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji,
ndiye atakayepanga ajenda, mahali na wakati wa kufanyika kwa mkutano wenyewe.
Katika miaka ya nyuma, zilikuwepo nyakati ambapo klabu
ilikaa hadi miaka mitatu pasipo kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wowote wa wanachama.
Hakuna mwanachama au kikundi chochote kilichojitokeza kudai mkutano wa dharura
wakati huo ingawa ilikuwa ikifahamika kwamba huo ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa
katiba ya klabu.
Tangu uongozi huu uingie madarakani takribani miaka mitatu
iliyopita, mikutano mikuu miwili ya wanachama imefanyika kwa mujibu wa KATIBA.
Mungu akijaalia, uongozi huu utafanya mkutano mwingine wa kawaida wa wanachama
baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kwa kuzingatia hali halisi ya klabu, Mwenyekiti
wa Simba, Alhaji Ismail Aden Rage (Mb), mwezi uliopita alitangaza dhamira yake
ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wakati wowote kuanzia sasa.
Rage alisema mkutano huo ungekuwa na ajenda moja tu;
Kujadili Mwenendo wa Klabu kwenye mashindano inayoshiriki msimu huu.
Kwa bahati mbaya, Mwenyekiti alishikwa na maradhi na
akapelekwa India
kwa matibabu na yuko huko hadi Mola atakapomjalia afya njema na kurejea. Kuna
uwezekano mkubwa, Inshallah, akarejea mwishoni mwa wiki ijayo.
Hii maana yake ni kwamba uongozi umeridhia kufanyika kwa
Mkutano wa wanachama. Kimsingi, kama uongozi
umeridhia, hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano mkuu mwingine.
Mwenyekiti ameruhusiwa kuitisha Mkutano Mkuu kwa sababu
alichaguliwa na wanachama na hivyo ana nguvu ya kisheria (locus standi) kufanya
hivyo. Hawa wengine wanaoitisha mkutano wana nguvu gani ya kisheria kufanya
hivyo? Walichaguliwa na nani kuwakilisha wanachama? Lini na wapi?
Uongozi pia unaweza kuitisha mkutano kwa vile wenyewe ndiyo
wenye leja ya wanachama. Klabu sasa ina database yake ya kompyuta inayotambua
wanachama walio hai na wasio hai.
Kwa kutumia database hiyo, uongozi huu unatambua wanachama
walio hai na wasio hai. Hakuna mtu mwingine yeyote, aliye nje ya uongozi huu
anayefahamu wanachama walio hai na wasio hai. Hao wanachama wanaoitana kufanya
mkutano, wamehakikiwa na nani kubaini uhalali wao huo?
Uongozi wa Simba
SC unaona kwamba wale
wanaolazimisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wana ajenda binafsi na si za maslahi
ya klabu. Kama kweli wangekuwa na nia njema na
klabu wangesubiri mkutano ambao utaitishwa punde.
Kwani, kuna uharaka gani wa kufanyika mkutano kesho? Kwanini
hawataki Mwenyekiti, ambaye wanachama walimpa mamlaka ya kuongoza klabu kwa
kipindi cha miaka minne, awepo kwenye mkutano huo?
Kwanini hawataki kuungana na wana Simba wengine kumwombea
Mwenyekiti kwa Mungu ili amwepushe na ugonjwa na kumrejesha salama hapa
nyumbani? Kwanini mikutano hii iitishwe katika kipindi ambacho uongozi
umefungua mikono yake na kukaribisha kila mmoja mwenye mapenzi mema na klabu
kuja kuchangia?
Kwenye macho ya Katiba ya Simba na sheria za Tanzania , huu
mkutano wa kesho ni batili na una lengo la kuleta vurugu na mifarakano kwenye
jamii na michezo kwa ujumla wake. Michezo ni amani na furaha na michezo si
vurugu.
Tayari uongozi wa Simba umetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi
na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na ubatili wa mkutano
huo. Tunapenda kuwaomba wanachama wetu wasiopenda fujo na vurugu kwenye michezo
kukaa mbali na mkutano huo kwa vile vyombo vya dola vitaufuatilia.
Uongozi hautajiingiza katika kutoa dhamana au msaada wa
namna yoyote kwa yeyote ambaye atachukuliwa hatua na vyombo vya dola kutokana
na kujihusisha na mkutano huo.
Pia, Simba
SC inatoa wito kwa vyombo vya
habari kuwa makini wakati vinaporipoti matukio ya vurugu kwenye michezo. Kabla
mtu hajahojiwa kujieleza kama mwanachama wa
Simba, ni vema kwanza akaonyesha kadi yake ya uanachama na risiti za malipo
yake.
Wakati mwingine, waandishi huwa tunawapa nafasi kwenye
vyombo vyetu vya habari watu ambao hawana mchango wowote kwenye kukuza michezo
bali kuleta vurugu. Kwanini, tungejiuliza, ni watu wale wale ambao kila mwaka
huonekana wakati wa vurugu na wakati wa amani huwa hawaonekani?
Kwanini, vyombo vyetu vinatoa nafasi kwa watu ambao lengo
lao ni kuhakikisha vilabu vyetu vinazidi kubaki nyuma, vinakuwa na vurugu kila
wakati na michezo inaonekana kama ni sehemu ya wahuni na watu wasio na
utaratibu?
Mpira bado haujaleta tija kubwa kwenye uchumi wa Tanzania na kunufaisha wachezaji kwa sababu baadhi
ya watu makini na makampuni makubwa yanaogopa kujiingiza kwenye michezo kwa
sababu ya tabia kama hizi.
Ni vema vyombo vya habari vikafanya jitihada kubwa katika
kuwatambua waleta vurugu, si katika klabu ya Simba pekee, bali kwenye sekta ya
michezo kwa ujumla, ili visiwape nafasi ya kuharibu na badala yake vitoe nafasi
kwa wale wenye lengo la kujenga.
Tunasisitiza, uongozi huu utaitisha Mkutano Mkuu wa
Wanachama Wote mara baada ya kurejea kwa Mwenyekiti.
Comments
Post a Comment